Viongozi wa G7 kuzijadili siasa za kimataifa
15 Aprili 2015Na baada ya kuwasili kwa Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani John Kerry, kundi hilo sasa limekamilika na linatarajiwa kuyaangazia masuala kadhaa muhimu yanayohusiana na diplomasia ya kimataifa.
Ikiwa ni siku ya pili ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa kundi la nchi saba zenye utajiri mkubwa wa kiviwanda, changamoto kadhaa za kidiplomasia zimo kwenye ajenda kuu.
Kinyume na ilivyo hali nzuri ya hewa inayowakaribisha wajumbe katika mkutano wa leo mjini Luebeck, “hali ya hewa katika siasa za kimataifa ni mbaya sana”. Amesema Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier. Steinmeier ameorodhesha mada kadhaa ambazo zinatarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo wa G7. "Tunaanza leo na msimamo kuhusu mazugnumzo yetu na Iran, lazima tujadili hali katika Mashariki ya Kati, na ISIS, kuhusu Iraq na Syria na hali inayoripotiwa kuendeleakubadilika nchini Yemen".
Waziri Steinmeier ameukaribisha uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliofikiwa siku moja kabla ambao uliweka marufuku utoaji wa silaha kwa viongozi wa waasi wa Houthi nchini Yemen, lakini akasema bado „ni mapema mno kufikia hali ambayo mzozo huo unaweza kupunguzwa na kupatikana ufumbuzi wa kisiasa. Masuala yanayohusiana na mabadiliko ya tabia nchi na mustakabali wa migogoro ya Asia na Afrika pia yatajadiliwa pamoja na usalama wa safari za majini.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry aliungana na Steinmeier katika kutoa kauli za mwanzo za siku ya pili ya mkutano huo. Kerry aliwasili leo asubuhi, siku moja baada ya Rais wa Marekani Barack Obama kukubali kuruhusu tathmini ya bunge ya makubaliano yoyote zaidi ya mpango wa nyuklia wa Iran. Hii itakuwa na maana kuwa vikwazo dhidi ya Iran vinaweza kuondolewa tu baada ya idhini ya Bunge kama Iran itayakubali masharti ya kupunguza shughuli zake za kinyuklia. "Suala kuu ni changamoto ya kumaliza mazungumzo na Iran, katika kipindi cha miezi miwili na nusu ijayo. Jana, kulikuwa na makubaliano yaliyofikiwa mjini Washington kuhusiana na mchango wa bunge. Tuna matumaini katika uwezo wetu kwa rais kufikia muafaka na hivyo kuufanya ulimwengu kuwa salama".
Steinmeier amesema makubaliano ya Bunge la Marekani huenda yakawa na athari fulani kuhusu kama makubaliano ya mwisho na Iran yataweza kufikiwa. Kundi la mataifa sita yenye nguvu ulimwenguni, China, Ufaransa, Urusi, Uingereza, Marekani na Ujerumani, linatarajia kuwa na mkataba wa mwisho ifikapo mwisho wa mwezi Juni
Mwandishi: Bruce Amani/DW/reuters/DPA
Mhariri: Gakuba Daniel