1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa EU waridhia kibali cha COVID-19 kwa usafiri

25 Mei 2021

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameafiki kibali cha kidijitali cha COVID-19 kwa wasafiri miongoni mwa mataifa wanachama kama hatua ya kuwezesha usafiri, utalii na kukuza uchumi wakati huu wa msimu wa joto.

https://p.dw.com/p/3tw4V
Brüssel EU Gipfel Treffen Außenpolitik
Picha: Yves Herman/AP Pictures/picture alliance

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameukaribisha mpango uliokubaliwa na wabunge wa umoja huo wiki iliyopita wa kuanzisha kibali cha COVID-19 kabla msimu wa joto kufikia kilele kwa lengo la kukuza usafiri, utalii na uchumi miongoni mwa nchi wanachama baada ya vikwazo vya kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona.

Kibali hicho kitatolewa kwa wakaazi wa Umoja wa Ulaya ambao watathibitisha kuwa wamechanjwa, au wamepona baada ya kuugua COVID-19 au wale ambao hawajaambukizwa. Kibali hicho cha kidijitali kinatarajiwa kuanza kutolewa kuanzia Julai mosi na kitazuia sharti la watu kupimwa au kuwekwa karantini wakitokea taifa nyingine.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana leo Jumanne kuchanga dozi zisizopungua milioni 100 za COVID-19 kwa nchi masikini ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. Umoja huo unatarajia kupokea zaidi ya dozi bilioni moja kutoka kwa kampuni nne za kutengeneza chanjo ifikapo mwisho wa mwezi Septemba. 

Msaada wa dozi milioni 100 za chanjo ya COVID-19 kwa nchi maskini

Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen akiwa amevalia barakoa alipowasili brussels kwa mkutano wa kilele Mei 24, 2021.
Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen akiwa amevalia barakoa alipowasili brussels kwa mkutano wa kilele Mei 24, 2021.Picha: Francisco Seco/AP Pictures/picture alliance

Wakikutana kwa siku mbili mjini Brussels, Ubelgiji kwenye mkutano wa kilele, viongozi wa nchi 27 za Umoja wa Ulaya wameunga mkono mpango ambapo wameahidi kuendelea na juhudi za kuongeza uwezo wa utengenezaji zaidi wa chanjo ulimwenguni kote ili kukidhi mahitaji ya chanjo. Hata hivyo haijabainika wazi ni aina gani ya chanjo miongoni mwa zilizopo AstraZeneca, Moderna, Pfizer na Johnson and Johnson watatoa kama msaada kwa nchi masikini.

Wametoa wito pia wa kuhakikisha usawa katika upatikanaji wa chanjo dhidi ya virusi vya corona. Wamesisitiza kujitolea kwao kuunga mkono mpango wa Umoja wa Mataifa wa ugavi wa chanjo kimataifa COVAX unaolenga kuhakikisha mataifa masikini na yenye mapato ya kadri pia yanapata chanjo.

Mpango huo ulipata pigo kubwa wiki iliyopita wakati India ambayo kampuni yake ya Serum Institute inatengeneza idadi kubwa ya chanjo kwa mpango huo, ilitangaza kuwa haitasafirisha chanjo nje ya India hadi mwisho wa mwaka kufuatia kuongezeka kwa maambukizi katika kanda hiyo ya bara Asia.

Kampeni ya chanjo yajikongoja katika nchi maskini

Nchi nyingi maskini zajikongoja kwenye kampeni za utoaji chanjo ya COVID-19 kwa sababu ya uhaba wa dozi.
Nchi nyingi maskini zajikongoja kwenye kampeni za utoaji chanjo ya COVID-19 kwa sababu ya uhaba wa dozi.Picha: Andreea Campeanu/Getty Images

Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen aliwasilisha mpango uliodokeza kuwa dozi milioni 300 zitakuwa zimewasilishwa kwenye umoja huo ifikapo mwisho wa mwezi huu hivyo asilimia 46 ya idadi jumla (sawa na watu milioni 450) wataweza kupata dozi ya kwanza.

Lakini wakati kampeni ya chanjo ikiendelea vyema miongoni mwa nchi za Magharibi, nchi maskini hali ni tofauti, nyingi zinahangaika hata kupata chanjo.

Makubaliano hayo yamejiri baada ya Marekani kusema mapema mwezi huu kuwa itatoa dozi milioni 20 zaidi kwa nchi masikini. Awali iliahidi kutoa dozi milioni 60 ya chanjo ya AstraZeneca.

Kuhusu mabadiliko ya tabianchi, viongozi wa nchi 27 za Umoja wa wa Ulaya wanajadiliana juu ya muongozo wa kufikia malengo yenye uzito wa kisheria, ya kushusha viwango vya utoaji wa gesi ya ukaa inayochafua mazingira. Umoja wa Ulaya unaazimia kupunguza viwango hivyo kwa asilimia 55 ifikapo mwaka 2030, ikilinganishwa na viwango vya mwaka 1990.

(APE, RTRE, AFPE)