Viongozi wa EU wakutana kujadili mfuko wa ufufuaji uchumi
17 Julai 2020Lakini hiyo sio hali pekee ambayo viongozi hao wanajikutana wakiwa mbali kutoka kila mmoja katika mkutano kama huo, lakini mpango wa bajeti ya Umoja wa Ulaya ya Trilioni 1.85 na mfuko wa ufufuaji uchumi unawaweka mbali mbali kimtazamo.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliongoza majadiliano ya mapema, akiwasili jana na kutumia saa za mwanzo kabla ya mkutano kukutana na waziri mkuu wa Uholanzi Mark Rutte, mtu mwenye msimamo mkali kabisa kuhusu kubana matumizi ya bajeti na anayeonekana kuwa mmoja kati ya kikwazo kikubwa katika kufikiwa makubaliano katika mkutano huo wa siku mbili.
Mkutano huo unaweza kuchukua muda mrefu zaidi, kama itakuwa muhimu, kuondoa tofauti zilizopo baina ya viongozi.
Changamoto zinazoyakabili mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya ni kubwa. Kundi hilo la mataifa linasumbuka kutokana na mdororo mbaya zaidi katika historia na mataifa wanachama yanapambana juu ya nani atalipa zaidi kusaidia mataifa mengine na mataifa gani yanapaswa kupata fedha zaidi ili kubadili mwelekeo wa uchumi wao ulioathirika.
Mzozo uliosababishwa na janga la virusi vya corona, pamoja na madhara yake yote ya kiuchumi na kijamii, ni mbaya sana ambao hatujawahi kukumbana nao tangu vita vikuu vya pili vya dunia," rais wa baraza la Ulaya na mwenyekiti wa mkutano huo Charles Michel amesema jana jioni.
Matumaini kwa Merkel
Wajumbe watapunguzwa kufikia tu idadi ya wastani, wakiachwa viongozi wakitegemea tu ujuzi wao binafsi katika maelezo ya waraka huo tata. Tangu kuzuka kwa janga la virusi vya corona kansela wa Ujerumani Angela Merkel , anaonekana kuwa ana uwezo wa kuiongoza nchi yake kupita katika mzozo huu na hivi sasa ikiwa Ujerumani inashikilia urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya, nafasi yake itakuwa kubwa zaidi katika mkutano huu. Alipowasili jana mjini Brussels alisema.
"Tunakutana leo kwa mara ya kwanza kuhuu suala la mfuko wa kufufua uchumi utakaotuwezesha kuwa imara kwa siku zijazo. Majadiliano yetu mwezi Februari hayakufikia mafanikio. Tumefanya matayarisho mengi lakini sasa tunajikuta katika hali tofauti na ilivyokuwa mwezi Februari. Na ndio sababu tunaingia katika majadiliano haya kwa matumaini makubwa , pamoja na kwamba tofauti zetu ni kubwa , lakini mara hii tutapata matokeo."
Mataifa wanachama walikuwa wakipambana vikali kuhusu bajeti ya miaka saba ya Umoja wa Ulaya ya trilioni 1.85 wakati COVID-19 ilikuwa ni taarifa ndogo tu kutoka Wuhan, China mwishoni mwa mwaka jana. Baada ya hapo virusi hivyo vilishambulia mataifa ya Umoja wa Ulaya kwa nguvu zote na makadirio hivi sasa ni kwamba uchumi wa mataifa 19 yanayotumia sarafu ya euro utanywea kwa asilimia 8.7 mwaka huu.