1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa EU wajaribu kupata muafaka wa ufufuaji uchumi

Sekione Kitojo
17 Julai 2020

Shinikizo linaongezeka kwa viongozi 27 wa Umoja wa Ulaya kufikia muafaka katika majadiliano yao makali yanayouusu pendekezo la mpango wa euro bilioni 750 wa kuufufua uchumi na bajeti ya umoja huo ya miaka saba ijayo. 

https://p.dw.com/p/3fVQZ
Belgien Brüssel EU-Gipfel | Sitzungssaal
Picha: Reuters/F. Lenoir

Nchi hizo  zina  mengi  ya  kupoteza  katika  mkutano  huu  wa kwanza  wa  ana kwa  ana  ambao  haujafanyika  katika  hali  hiyo kwa  miezi  kadhaa. Kundi  hilo  la  mataifa  linakabiliwa  na  mdororo mkubwa  kabisa  wa  ukuaji  wa  uchumi  tangu  umoja  huo kuundwa, na  mataifa  yanahitaji  fedha  haraka  kujitoa kutoka katika  mzozo  wa  kiuchumi uliosababishwa na  janga  la  ugonjwa wa  COVID-19..

Belgien  EU Ratsitzung  Treffen EU Rat Brüssel
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akiwa na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron Picha: Reuters/S. Lecocq

Wakati  viongozi  kadhaa  wameeleza  matumaini  yao  kupatikana muafaka  wakiwa  njiani  kuelekea  katika  mkutano  huo wa  kilele, uwezekano  halisi  wa  kufikiwa  makubaliano  leo Ijumaa  ama kesho Jumamosi yanaonekana  yameporomoka  kwa  Ujerumani.

Leo Ijumaa, akiwa  ni  siku  yake  ya  kuzaliwa  akitimiza  miaka  66, kansela  Angela  Merkel  amesikika  akiwa hana imani  ya  kutosha kwamba  mkutano  huo  wa  kilele  utapata  ufumbuzi  kuhusu  mfuko wa  bilioni  kadhaa  wa  ufufuaji  wa  uchumi  wakati huu wa  janga  la virusi  vya  corona.

"Niseme tu kwamba  tofauti  bado  ni  kubwa  sana. Kwa hiyo  siwezi kusema  iwapo tutapata matokeo mara hii," Merkel  aliwaambia waandishi  habari  mjini  Brussels. Unapaswa kukabiliana na hali halisi."

Belgien Brüssel EU-Gipfel | Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani aliyetimiza umri wa miaka 66 leo anamatumaini madogo ya kupatikana muafaka.Picha: Getty Images/AFP/F. Seco

Muda wa ukweli

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron  alisema "ana matumaini  lakini ya tahadhari" kwamba  makubaliano  yanaweza  kufanyika, "ni  muda wa  ukweli  na  dhamira kwa  Ulaya."

Merkel  na  Macron  wote walifanya  mikutano na  viongozi mbalimbali katika wiki  za  hivi  karibuni  na  wamechukua  jukumu  la mbele  katika  kutoa  rai kwa  mawaziri  wakuu  kufikia  maridhiano.

Msingi wa  majadiliano  hayo  ni  pendekezo la  rais  wa  Baraza  la Umoja  wa  Ulaya,  Charles Michel   ambalo  linalenga  kiwango  cha euro  bilioni 500 za misaada  na  euro bilioni  250  za mikopo, hoja hiyo  ikiwa  katika  msingi wa  pendekezo  la  hapo  kabla  na Halmashauri  ya  Umoja  wa  Ulaya.

Brüssel EU Indien Videokonferenz Modi, Michel und von der Leyen
Rais wa Halamshauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen (kushoto) na rais wa baraza la Ulaya Charles Michel(kulia)Picha: Reuters/Y. Herman

Alipoulizwa  iwapo pendekezo hilo linaweza kupita kirahisi, Rais wa  Bunge  la  Ulaya, David Sassoli  alisema, "Umoja  wa  Ulaya  si mashine  ya  benki (ATM), tuna kitu  zaidi  cha kusema, sio tu  kama watu  wa  Ulaya,  lakini  pia mataifa wanachama. Tuna  kitu  zaidi  kuliko kujiangalia  tu  kama  wagawa fedha. Tuna jukumu  kubwa  kuurejesha  uchumi  katika  hali  ya kawaida, kuhakikisha  hali  bora za raia wetu, uhuru  wa maoni ya umma, na kufanya kwa mpango ambao  utaruhusu  Umoja wa Ulaya kulinda maadili  yake."

Afisa  huyo  mwandamizi  wa Umoja  wa  Ulaya  ameongeza  kuwa makubaliano  yanawezekana  iwapo  viongozi wataweza  kupata hamasa ya kisiasa  kufanya  hivyo.