Viongozi wa ECOWAS wakutana tena
3 Mei 2012Mkutano wa ECOWAS, unafanyika wiki moja baada ya kuwepo kwa mkutano mwingine wa aina hiyo ambapo wakuu wa nchi zinazounda jumuiya hiyo walijadili kuhusu hali ya usalama ya Mali na Guinea Bissau. Rais Macky Sall wa Senegal ndiye aliyeufungua mkutano wa leo uliohudhuriwa na viongozi 12 kati ya 15 wa nchi za ECOWAS. Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, rais Allasane Ouattara wa Cote D'Ivoire amelaani hatua ya wanajeshi wa Mali na Guinea Bissau kukataa maamuzi ya ECOWAS.
Katika mkutano unaofanyika leo, ECOWAS itayatathmini mambo yanyaoendelea Guinea Bissau hivi sasa kufuatia kundi la mawaziri wa mambo ya kigeni wa jumuiya hiyo kushindwa kufikia muafka na utawala wa kijeshi juu ya kufuata mpango wa serikali ya mpito wa miezi 12. Mazungumzo hayo yalilenga kuandaa njia kwa ajili ya Guinea Bissau kurejea katika utawala wa kikatiba baada ya serikali iliyokuwa ikiiongoza nchi hiyo kupinduliwa tarehe 12 Aprili. ECOWAS imemlaumu kiongozi wa mapinduzi, Antonio Indjai kuuwa ndiye aliyepelekea jumuiya hiyo na watawala wa kijeshi kutokufikia makubaliano.
Machafuko yaendelea Mali
Viongozi wa ECOWAS watazungumzia pia hali ilivyo hivi sasa nchini Mali ambapo hali inazidi kuwa tete baada ya vikosi vitiifu kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Amadou Toumani Toure, kushindwa kuupindua utawala wa kijeshi uliopo madarakani sasa. Toure aling'olewa madarakani katika mapinduzi yaliyofanyika mwezi Machi mwaka huu. Lakini sasa watu walioipindua serikali wameafiki kuyakabidhi madaraka kwa rais wa kipindi cha mpito, wakifuata makubaliano yaliyoandaliwa na ECOWAS.
Hata hivyo machafuko yamekuwa yakiendelea katika mji mkuu wa Mali, Bamako, na wahudumu wa hospitali wameliambia shirika la habari la AFP kwamba watu wasiopungua 22 wameuliwa katika mapigano kati ya viongozi wa kijeshi na vikosi vitiifu kwa Amadu Toumani Toure.
Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Afrika Magharibi, Said Djinnit, amelaani machafuko yaliyotokea hivi karibuni huko Mali na kusema kwamba machafuko hayo yanaongeza ugumu wa kipindi hiki cha mpito. Licha ya kwamba wanajeshi hawapo madarakani tena, nguvu yao bado ni dhahiri. Kapteni Sanogo aliyeongoza mapinduzi, amekataa wito wa ECOWAS wa kuitisha uchaguzi katika kipindi cha miezi 12 ijayo na kutuma kikosi cha kusimamia amani.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman