Viongozi watofautiana kuhusu waranti wa kukamatwa Netanyahu
22 Novemba 2024Matangazo
ICC pia ilitoa waranti za kukamatwa waziri wa zamani wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant na mkuu wa kijeshi wa Hamas Mohammed Deif. Zilitolewa kuhusiana na tuhuma za uhalifu dhidi ya ubinaadamu na uhalifu wa kivita katika vita vya Israel dhidi ya Hamas huko Gaza, vilivyochochewa na shambulizi la kundi hilo la wanamgambo wa Kipalestina la Oktoba 7, 2023 dhidi ya Israel.
Netanyahu ameutaja uamuzi wa ICC kuwa ni wa chuki dhidi ya Wayahudi. Marekani pia imeupinga uamuzi huo. Naye Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borell amesema uamuzi huo wa ICC lazima uheshimiwe na kutekelezwa. Mamlaka ya Palestina, ambayo ni mpinzani wa Hamas imeukaribisha uamuzi huo ikisema unawakilisha matumaini na imani kwa sheria za kimataifa na taasisi zake.