1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa dunia wamuaga Helmut Kohl

1 Julai 2017

Umoja wa Ulaya umetoa heshima za mwisho kwa kansela wa zamani wa Ujerumani Helmut Kohl, mmoja wa waasisi wa Ulaya ya sasa, katika sherehe ya iliyohudhuriwa na viongozi kadhaa wa dunia, wa sasa na wa zamani.

https://p.dw.com/p/2fksV
Straßburg Trauerfeier Europa nimmt Abschied von Helmut Kohl Bill Blinton
Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton akizungumza mjini Strasbourg katika sherehe ya kumuaga hayati Helmut Kohl, 01.07.2017.Picha: picture alliance / Sven Hoppe/dpa

Kohl ambaye alisimamia kuungana tena kwa Ujerumani na alikuwa kinara wa muungano wa Ulaya, alifariki June 16 akiwa na umri wa miaka 87. Sherehe za siku nzima za kumuaga zilianzia katika makao makuu ya bunge la Ulaya mjini Strasbourg, na zitahitimishwa kwa maziko ya faragha yatakayofanyika katika mji wa Speyer nchini Ujerumani. Mke wake aliomba kusiwepo na maziko ya kitaifa kwa hayati Kohl.

Jeneza la kansela huyo wa zamani liliwasilishwa katika ukumbi wa bunge mjini Strasbourg ambako mrithi wake, Kansela Angela Merkel, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton wametoa hotuba. Waziri Mkuu Dmitry Medvedev ameiwakilisha Urusi katika sherehe hizo, ambazo zimehudhuriwa pia na waziri mkuu wa Uingereza Theresa May, na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Chimbuko halisi la Ulaya

Trauerfeierlichkeiten für Altkanzler Kohl
Kansela Angela Merkel akitoa heshima zake kwa jeneza la hayati Helmut Kohl mjini Strasbourg, 01.07.2017.Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Euler

Hotuba hizo na filamu fupi itakayoonyeshwa kwa waombolezaji vinajikita katika mchango wa Kohl katika kuiunganisha tena Ujerumani baada ya kuanguka kwa ukuta wa Berlin mwaka 1989, na katika ushirikiano wake na rais wa zamani wa Ufaransa Francoise Mitterand katika kuunda Umoja wa Ulaya. Hii ndiyo mara ya kwanza kwa bunge la Ulaya kutoa heshima kwa kiongozi kwa namna hiyo.

Wazo la sherehe hiyo lilitolewa na rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker, ambaye Kohl alikuwa akimuita "Junior" wakati alipochaguliwa kuwa waziri mkuu wa Luxembourg akiwa na umri wa miaka 41. Wakati Kohl alipofariki, Juncker alimuelezea kama "Mnasihi wangu, rafiki yangu, na chimbuko halisi la Ulaya."

Jengo la bunge katika mji wa Strasbourg ulioko katika eneo la mpakani mwa Ufaransa na Ujerumani limezungushiwa na chuma, huku askari polisi zaidi ya 2000 wakiwekwa kuhakikisha usalama wa wageni. Baada ya sherehe mjini Strasbourg, jeneza la Kohl litasafirishwa kwa helikopta kwenda mji wa Ludwigshafen ambako utahamishiwa katika boti na kupelekwa kupitia Mto Rhein hadi kwenye mji wa kusini-magharibi wa Speyer kwa ajili ya mazishi.

Mgogoro ndani ya familia

Lakini utaratibu huo umekosolewa na mtoto mkubwa wa Kohl. Katika mahojiano na gazeti la kila wiki la Ujerumani - Die Zeit, aliitaja mipango hiyo kuwa isiyowiana na mchango wa baba yake katika historia ya Ujerumani. Walter Kolh, ambaye mama yake alikuwa mke wa kwanza wa kansela huyo wa zamani Hannelore Kohl, alikosoa kutokuwepo mazisha ya kitaifa, yaliokataliwa na mke wa pili wa Kohl Maike Kohl-Richter.

Kohl alimuoa Kohl-Richter, ambaye ni mdogo kwake kwa miaka 34, alipokuwa na umri wa miaka 78. Moja wa sababu za bibi Richter-Kohl kukataa mazishi ya kitaifa ni hasira zilizoendelea kuwepo kuhusu namna Merkel alivyomtendea Kohl ambaye ni mnasihi wake wa zamani. Merkel alimuondoa Kohl kwenye uongozi wa chama cha Christian Democratic Union CDU, na kukitaka chama kumfuta alipokumbwa na kashfa kuhusu ufadhili wa chama.

Trauerfeierlichkeiten für Altkanzler Kohl
Rais wa halmashauri kuu ya Ulaya Jean-Claude Juncker (kushoto) akimuangalia waziri mkuu wa Uingereza Theresa May wakati akiwasili katika ukumbi wa bunge mjini Strasbourg kwa ajili ya sherehe ya kumuaga Kohl. Viongozi wa sasa na zamani wamehudhuria.Picha: picture-alliance/AP Photo/J.-F. Badias

Walter Kohl anataka jeneza la baba yake lipelekwe katika mji mkuu wa Ujerumani Berlin kwa ajili ya kuagwa kitaifa, kufanyiwa ibada ya misa na sherehe ya kuagwa kijeshi karibu na lango la Brandenburg, ambako kiongozi huyo wa Ujerumani alishuhudia kuanguka kwa ukuta wa Berlin.

Kutokana na mgogoro wa muda mrefu na mama yake wa kambo, ambaye anaulinda kwa ungalifi mkubwa urithi wa kisiasa wa mume wake, Walter Kohl hakuwa na mawasiliano na baba yake kwa miaka mingi, na alisema alijua kuhusu kifo chake kupitia taarifa za redio.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,dpae

Mhariri: Daniel Gakuba