Viongozi wa dunia walaani shambulio la Uingereza
23 Machi 2017Katika taarifa nje ya ofisi yake ilioko Mtaa wa Downing, waziri mkuu wa Uingereza Theresa May alilielezea shambulio hilo kuwa la kuchukiza na potovu, na kusema kuwa mshambuliaji huyo alichaguwa eneo la bunge kama mashambulizi dhidi ya maadili ya kidemokrasia ya Uingereza.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema Ujerumani inasimama thabiti na imara pamoja na Waingereza katika mapambano dhidi ya aina zote za ugaidi, huku rais Frank-Walter Steinmeier akiongeza kuwa: "Katika nyakati hizi za hatari, sisi Wajerumani tuko karibu zaidi na watu wa Uingereza.
Rais wa Ufaransa Francois Hollande alituma ujumbe wa mshikamano na kuunga mkono watu wa Uingereza, akisema Ufaransa inaelewa maumivu yao baada ya shambulio hilo, ambamo wanafunzi watatu wa Kifaransa walijeruhiwa pia.
Ikulu ya Marekani pia ililaani shambulio hilo na kuahidi msaada kamili wa serikali ya Marekani katika kujibu shambulio hilo na kuwafikisha wahusika mbele ya sheria, alisema Sean Spicer, msemaji wa ikulu hiyo ya White House mjini Washington.
Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau aliandika kwenye ukurasa wake wa twita kuwa: Hisia zetu ziko pamoja na waathirika wa shambulio la London pamoja na familia zao. Wacanada wanaendelea kuwa pamoja na watu wa Uingereza.
Juncker: Ni ugaidi
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker, alisema shambulio limemkumbusha Brussels, ambako magaidi wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu waliuwa watu 32 katika mashambulizi mawili dhidi ya uwanja wa ndege na kito cha reli mwaka mmoja uliopita.
"Hili ni shambulio la kigaidi na halibadilishi chochote kwa walioathirika. Tuko pamoja na waathirika, na hii ni siku maalumu mjini Brussels, nchini Ubelgiji, kwa sababu mwaka mmoja uliopita, mwaka mmoja kamili uliopita, tulikuwa na mashambulio mjini Brussels," alisema Junckers mjini Brussels alikokuwa kuadhimisha mwaka mmoja tangu mashambulizi ya 2016.
Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk alisema kupita ukurasa wake wa twitter kuwa Ulaya inasimama pamoja na Uingereza dhidi ya ugaidi na iko tayari kusaidia. Urusi nayo kupitia msemaji wa wizara yake ya mambo ya nje ilituma ujumbe wa rambirambi. Waziri mkuu wa Uholanzi Mark Rutte aliiambia televisheni ya Kidachi kwamba alistushwa na habari za kutisha na kusema wanaomboleza pamoja na London.
Waziri Mkuu wa Italia Paolo Gentilon, ambaye alinyamaza kwa muda mwanzoni mwa mkutano wa wabunge wa chama cha Social Democratic, alituma salamu za rambirambi pia. Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisisitiza kuwa Uturuki inahisi na kushiriki kikamilifu katika maumivu ya Uingereza na inasimama pamoja na nchi hiyo katika mapambano dhidi ya ugaidi.
Mawaziri wakuu wa uhispania Mariano Rajoy, wa Australia Malcom Turnbull, wa China Li Keqiang na wizara ya mambo ya nje ya Singapore wote waliezelea mshikamano na Uingereza, huku Qatar ikisisitiza msimamo wa kupinga vurugu za kila aina na kuelezea kuiunga mkono Uingereza katika hatua zake zote za kuhakikisha usalama katika wakati huu mgumu. Rais wa Venezuela Nicolas Maduro pia alisema anaungana na watu wa London na kupinga aina zote za ugaidi.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,ape.
Mhariri. Daniel Gakuba