1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G20 waanza Uturuki

15 Novemba 2015

Viongozi wa dunia wamekusanyika kwa mkutano wa kilele nchini Uturuki kutoa ujumbe wa umoja baada ya mashambulizi mjini Paris.

https://p.dw.com/p/1H60a
Türkei Antalya G20 Gipfel
Mkutano wa G20 nchini UturukiPicha: Getty Images/C. McGrath

Viongozi hao lakini watajishughulisha pia na mtengano mkubwa kuhusiana na mizozo mbali mbali inayosababisha Syria kutengana.

Rais wa Marekani Barack Obama , rais wa China Xi Jinping na Vladimir Putin wa Urusi watajiunga na viongozi wengine katika mji wa kitalii wa kusini katika bahari ya Mediterania wa Antalya chini ya siku mbili baada ya mashambulizi yanayadaiwa kufanywa na kundi la Dola la Kiislamu kuwauwa kiasi ya watu 129 na kusababisha wimbi la mshutuko duniani kote.

Frankreich Paris Terroranschläge Trauer
Waombolezaji wakiweka maua katika eneo la shambulio mjini ParisPicha: DW/G. Matthes

Mtazamo wa mkutano huu wa kilele wa kundi la mataifa yaliyoendelea na yale yanayoinukia kiviwanda yaani G20 umebadilishwa na mashambulizi hayo, ambapo usalama na mzozo wa Syria hivi sasa vinagubika ajenda ya kawaida ya kifedha ambapo italazimika pia kushughulikia suala la kusambaa kwa mzozo wa wakimbizi, mabadiliko ya tabia nchi na ukwepaji wa kodi.

Afisa katika ujumbe wa Ufaransa katika mkutano huo, unaoongozwa na waziri wa mambo ya kigeni Laurent Fabius baada ya rais Francois Hollande kuamua kubaki nyumbani kuliongoza taifa hilo lililojawa na fadhaa , amesema inatarajiwa kwamba wakati wa mkutano huo "kutakuwa na msisitizo maalum kuhusu ugaidi".

Frankreich Paris Terroranschläge Trauer
Maua katika eneo la tukio mjini ParisPicha: DW/L. Scholtyssyk

Obama na Putin ana kwa ana

Mkusanyiko huo wa viongozi unatoa uwezekano wa kwanza wa mkutano kati ya Obama na Putin tangu Urusi kuanzisha mapambano yake ya anga nchini Syria dhidi ya Dola la Kiislamu , ambapo mataifa ya magharibi yanashaka kwamba yanalenga katika kuusaidia utawala wa rais Bashar al-Assad.

Ikulu ya Marekani ya White House imesema inawezekana kuwapo na mkutano ambao sio rasmi baina ya viongozi hao wawili , ambao mahusiano yao katika mikutano ya hapo kabla imeteka vichwa vya habari mbali ya matamshi yao.

Hakuna mkutano rasmi unaotarajiwa hata hivyo.

Türkei G20 Gruppenbild
Viongozi wa mashirika mbali mbali ya dunia katika mkutanoPicha: picture-alliance/AP Photo/B. Ozbilici

Mwenyeji wa mkutano huo , rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan , ambae anataka kuutumia mkutano huo wa kilele kuimarisha hadhi yake kama kiongozi wa dunia baada ya kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mwezi huu, ametoa wito kwa dunia kupata kile alichokiita " makubaliano imara" kuhusiana na ugaidi yanapotokea mashambulizi.

Lakini pamoja na kuwa na viongozi kama Putin na Obama hakutakuwa na matatizo kusimama pamoja katika kulaani kwa pamoja ugaidi, lakini kuondoa tofauti kuhusu Syria litakuwa jambo gumu sana.

Matukio yote yanayojumuisha muziki, ikiwa ni pamoja na chakula rasmi cha usiku , yamefutwa kama ishara ya heshima kwa wahanga wa shambulio la mjini Paris katika mkutano huo wa kilele, ambao unaanza rasmi mchana leo Jumapili , zimesema duru katika ofisi ya rais wa Uturuki.

Russland Putin und Mutko
Rais Putin wa Urusi (kulia)Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Druzhinin

Viongozi hao watapata taabu bila shaka kutafuta msimamo wa pamoja kuhusiana na mzozo wa Syria, ambapo mwenyeji Uturuki inapinga vikali mashambulizi ya anga ya Urusi na kupata tu jibu la juu juu kuhusiana na pendekezo lake la kuweka eneo salama ambalo wapiganaji wa jihadi wa Dola la Kiislamu hawataweza kulifikia , eneo litakaloundwa ndani ya Syria kama sehemu salama kwa wakimbizi.

"Naomba na nina matumaini kwamba kundi la G20 litatoa jukwaa ambalo masuala haya yote yataweza kujadiliwa kwa uwazi na kisha tutaweza kuelewana, Erdogan amesema kabla ya mkutano huo.

Dunia yaonesha mshikamana na Paris

Wakati huo huo wimbo wa "La Marseillaise" ulitamba jana Jumamosi kutoka Dublin hadi New York wakati maeneo muhimu duniani yakiwekwa bendera zenye rangi ya taifa la Ufaransa na maelfu wakiandamana kuonesha mshikamano na mji wa Paris baada ya mashambulizi ambayo yamesababisha watu 129 kuuwawa.

Frankreich Terror in Paris Reax Obama
Rais Obama wa MarekaniPicha: Getty Images/AFP/J. Watson

Maeneo kama Sydney Opera House nchini Australia hadi One World Trade Center mjini New York yaliwekwa bendera za rangi nyekundu, nyeupe na buluu, wakati ishara ya "amani kwa Paris" ikiwa pamoja na ishara ya jiji la Paris ya mnara wa Eiffel pamoja na ishara ya amani ya miaka ya 1960 ikitumika kila mahali.

Na polisi ya Ubelgiji imewakamata watu watatu jioni ya Jumamosi(14.11.2015) kwa kuhusika katika mashambulizi hayo ya kumwaga damu ya kigaidi katika nchi jirani ya Ufaransa, ambapo kundi lenye itikadi kali la Dola la Kiislamu limedai kuhusika.

Polisi imemkamata raia wa Ufaransa anayeshukiwa kukodi gari iliyopatikana karibu na eneo la tukio la mashambulizi mjini Paris, wakati akiwa anaendesha gari nyingine katika kitongoji cha Molenbeek, waziri wa sheria Koen Geens amekiambia kituo cha utangazaji cha RTBF.

Watu wawili wanaume raia wa Ubelgiji pia wamekamatwa.

Raia huyo wa Ufaransa anafahamika na maafisa wa Ubelgiji ambao wamekuwa wakifuatilia shughuli za kaka yake, Geens amesema.

Waziri mkuu wa Ubelgiji Charles Michel amekiambia kituo cha televisheni cha RTL kwamba mmoja kati ya watu hao waliokamatwa katika kitongoji cha Molenbeek anafikiriwa alikuwa mjini Paris siku ya Ijumaa usiku, kabla ya kukiambia kituo kingine cha RTBF baadaye kwamba hilo bado linachunguzwa.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe

Mhariri: Isaac Gamba