1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa dunia wajiunga na maandamano dhidi ya ugaidi

11 Januari 2015

Viongozi wa dunia wameshikana mikono kuwaongoza mamia ya wananchi wa Ufaransa katika maandamano yaliokuwa chini ya ulinzi mkali kutowa heshima zao kwa wahanga wa mashambulizi ya wanamgambo wa Kiislamu wa itikadi kali.

https://p.dw.com/p/1EIfI
Rais Ibrahim Boubacar Keita wa Mali(kulia), Rais wa Ufaransa Francois Hollande(katikati) na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani wakiwa mstari wa mbele katika maandamano dhidi ya ugaidi Paris. (11.01.2015)
Rais Ibrahim Boubacar Keita wa Mali(kulia), Rais wa Ufaransa Francois Hollande(katikati) na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani wakiwa mstari wa mbele katika maandamano dhidi ya ugaidi Paris. (11.01.2015)Picha: picture-alliance/dpa/Hoslet

Rais Francois Hollande wa Ufaransa aliandamana bega kwa bega na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron ambao walikuwa mstari wa mbele pamoja na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas.

"Paris leo ni mji mkuu wa dunia" amesema hayo Rais Hollande kabla ya kuanza safari ya maandamano yaliohudhuriwa na watu milioni moja na nusu mjini Paris.Maandamano kama hayo ya kulaani ugaidi yamefanyika katika miji mengine nchini kote Ufaransa na Ulaya.

Polisi na wanajeshi wanaofikia 2,200 walikuwa katika doria kwenye mitaa ya Paris kuwalinda waandamanaji dhidi ya uwezekano wa kushambuliwa huku polisi wa kulenga shabaha wakiwa wamemwagwa kwenye mapaa ya nyumba na askari kanzu wakichanganyika na umati wa watu.

Maandamano makubwa kabisa

Maandamano hayo ambayo yumkini yakawa ndio maandamano makubwa kabisa katika historia ya kisasa kufanyika Paris yanaonyesha fadhaa iliyotokana na shambulio baya kabisa la wanamgambo wa Kiislamu wa itikadi kali kuwahi kushuhudiwa katika mji mkuu wa Ulaya katika kipindi cha miaka tisa.

Umma uliomiminika katika maandamano Paris.(11.01.2015)
Umma uliomiminika katika maandamano Paris.(11.01.2015)Picha: Reuters/Platiau

Kwa Ufaransa yamezusha masuala ya uhuru wa kujieleza,dini na usalama na kutoka nje ya mipaka ya Ufaransa mashambulizi hayo ya kigaidi yameonyesha urahisi wa kufanyika kwa mashambulizi hayo mijini.

Watu wawili waliohusika na mashambulizi hayo wametangaza utiifu wao kwa kundi la Al Qaeda lilioko Yemen na mshambuliaji wa tatu ametangaza utiifu wake kwa kundi la Dola la Kiislamu.

Mashambulizi mabaya

Watu 17 wakiwemo waandishi na polisi wameuwawa katika siku tatu za matumizi ya nguvu ambayo yalianzia na shambulio la mauaji dhidi ya ofisi ya gazeti la kila wiki la Charlie Hebdo linalojulikana kwa tashtiti zake kwa Uislamu na dini nyengine pamoja na wanasiasa.

Sehemu ya waandamanaji Paris. (11.01.2015)
Sehemu ya waandamanaji Paris. (11.01.2015)Picha: picture-alliance/dpa/Fredrik von Erichsen

Taharuki hiyo ilimalizika Ijumaa kwa ushikiliaji wa mateka katika duka moja la Kiyahudi ambapo mateka wanne waliuwawa pamoja na mhusika wa kisa hicho ambaye aliuliwa na polisi.

Muda mfupi kabla ya kuanza kwa maandamano kumeibuka mkanda wa video wenye kumuonyesha mwanaume anayefanana na yule aliyehusika na kisa cha kuwashikilia watu mateka katika duka la Kiyahudi akiahidi utiifu wake kwa uasi wa Dola la Kiislamu na kuwataka Waislamu wa Ufaransa kufuata mfano wake.

Hisia tafauti

"Hatutokubali kuliachia genge la wahuni kuyaendesha maisha yetu" hayo yametamkwa na Fanny Applebaum mwenye umri wa miaka 75 ambaye amesema alipoteza dada zake wawili na kaka mmoja katika kambi ya mateso ya Manazi huko Auschwitz.Amesema "Leo sote ni kitu kimoja".

Zakaria Moumni raia wa Ufaransa mwenye asili ya Moroco ambaye ana umri wa miaka 34 aliyejifunika kwa bendera ya Ufaransa amekubaliana na kauli hiyo kwa kusema kwamba " Niko hapa kuwaonyesha magaidi hawakushinda....ni kuwajumuisha pamoja watu wa dini zote."

Miongoni mwa watoto wengi waliopelekwa kwenye maandamano hayo ni Loris Peres mwenye umri wa miaka 12 aliyesema "Kwangu mimi huku ni kutowa heshima kwa watu unaowapenda ni kama familia ......tuliwahi kuwa na somo kama hilo shuleni."

Muandamanaji akiwa na bango la " Sisi ni Charlie."
Muandamanaji akiwa na bango la " Sisi ni Charlie."Picha: Reuters/Noble

Wakati kukukiwa na mshikamano mkubwa na wahanga pia kumekuwepo na sauti za upinzani.Mitandao ya kijamii nchini Ufaransa imekuwa na matamshi kutoka kwa wale ambao wana mashaka na kauli mbiu ya "Je suits Charlie" ikitafsiriwa kama ni uhuru wa kujieleza kwa gharama zozote zile. Wengine wanashuku kwamba kuna unafiki kwa viongozi wa dunia wanaohudhuria maandamano hayo ambao nchi zao zina sheria za kukandamiza vyomvbo vya habari.

Watu 12 waliuwawa katika shambulio la kwanza Jumatano dhidi ya ofisi ya gazeti la Charlie Hebdo kijarida kinachojulikana kwa kwa kuzitashtiti dini na wanasiasa.Washambuliaji ndugu wawili wazalia wa Ufaransa wenye asili ya Algeria wameshambulia ofisi ya jarida hilo kwa kuchapisha katuni zenye kumfananiza na kumdhihaki Mtume Muhammad (SAW).

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri : Bruce Amani