Viongozi wa dunia waadhimisha miaka 75 ya kuundwa UN
22 Septemba 2020Katika tukio la Umoja wa Mataifa kufikisha miaka 75 tangu kuundwa, kansela wa Ujerumani Angela Merkel jana alitoa wito wa mageuzi katika taasisi hiyo ya kimataifa pamoja na umoja mkubwa zaidi baina ya wanachama wake.
Mwishoni Umoja wa Mataifa unaweza kuwa kituo kizuri tu iwapo wanachama wake watakuwa na umoja," Merkel alisema katika ujumbe wa vidio aliotoa jana jioni katika sherehe za kuadhimisha miaka 75 tangu kuundwa kwa Umoja wa Mtaifa.
"Wale wanaoamini kwamba wanaweza kufanya vitu vyao vizuri zaidi peke yao wanakosea. Mfano uliopo ni janga la COVID-19 ambalo limeonesha kwamba matatizo ya dunia yanahitaji uelewa na ushirikiano kupindukia mipaka ya nchi katika kila eneo. Mwishoni mwa siku, Umoja wa Mataifa unaweza kufanya kazi vizuri zaidi iwapo wanachama wake watakuwa na Umoja."
Kansela amesemaMara nyingi baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakwama wakati uamuzi wa wazi unahitajika," akilizungumzia tawi hilo la Umoja wa Mataifa lenye jukumu la kuhakikisha kuwa amani ya kimataifa na usalama inapatikana. "Tunahitaji mageuzi."
Maslahi binafsi
Merkel pia alisema maslahi binafsi ya wanachama mmoja mmoja mara nyingi yanasababisha shirika hilo kushindwa kufanikisha malengo yake.
Naye katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kurejeshwa hali ya muungano zaidi, ambao ni msingi Umoja wa Mataifa. Wito huo umerudiwa na viongozi kubwa na ndogo , masikini na tajiri duniani kote.
Lakini licha ya kuwapo hotuba za kutia moyo , ni dhahiri kwamba changamoto bado ziko katika kuungana na kupambana na janga la virusi vya corona, pamoja na mizozo kadhaa midogo kuanzia mashariki ya kati hadi Afrika, na kufikia malengo ya Umoja wa mataifa ya kufuta umasikini uliokithiri na kulinda mazingira na kufikia lengo lililowekwa la mwaka 2030.
Mijadala ya kila mwaka ya baraza kuu la Umoja wa mataifa inaanza rasmi leo, ambapo viongozi wa dunia watatoa hotuba zao kupitia vidio badala ya kukusanyika mjini New York. Hii ni mara ya kwanza kufanyika hivyo kutokana na janga la virusi vya corona.