1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Catalonia wafika mahakamani Madrid

Sylvia Mwehozi
2 Novemba 2017

Viongozi kadhaa wa serikali ya Catalonia waliofukuzwa kazi, leo wamewasili katika mahakama ya kitaifa mjini Madrid wakikabiliwa na uwezekano kushtakiwa  kwa uasi na matumizi matumizi mabya ya fedha.

https://p.dw.com/p/2mtPB
Spanien Madrid Hoher Gerichtshof  Entlassene katalonisches Kabinettsmitglieder Meritxell Borras
Picha: Reuters/S. Vera

Wanasiasa 20 wa jimbo hilo akiwemo rais wa serikali ya jimbo hilo aliyefutwa kazi Carles Puigdemont, waliitwa mahakamani baada ya mwendesha mashitaka mkuu kusema washitakiwe kwa uasi, na matumizi mabaya ya fedha baada ya bunge la Catalonia kutangaza kujitenga Oktoba 27.

Uhispania ilichukua hatua ya kuchukua udhibiti wa Catalonia kufuatia tangozo la kujipatia uhuru na baadae kulifuta baraza la mawaziri, na bunge la jimbo hilo na kuitisha uchaguzi wa mapema Desemba 21.

Puigdemont, ambaye alikimbilia nchini Ubelgiji na viongozi wengine wa zamani wa baraza lake, atasalia nchini humo na hatohudhuria mahakamani, kwa mujibu wa mwanasheria wake, jambo ambalo litachochea kutolewa kwa waranti ya kumkamata na ombi la kurejeshwa.  Puigdemont alisema jana Jumatano kuwa atapuuza amri ya mahakama ya kujibu mashitaka juu ya dhamira ya jimbo hilo kujitangazia uhuru, akisema yuko tayari kutoa ushahidi akiwa nchini Ubelgiji, ambako amesafiri akiwa na viongozi wengine wanne wa baraza la mawaziri waliofukuzwa.

Pressekonferenz Puigdemont Brüssel
Carles Puigdemont akizungumza na waandishi wa habari mjini BrusselsPicha: Reuters/Y. Herman

Kundi la viongozi wa walioitwa mahakamani ni pamoja na wanachama 13 wa baraza la zamani la mawaziri na wabunge 6. Makamu wa rais wa zamani wa Puigdemont, Oriol Jungeeras alikuwa wa kwanza kuwasili katika mahakama ya kitaifa, akisindikizwa na wanasheria na kukataa kusema chochote mbele ya waandishi wa habari.

Chini ya sheria za Uhispania, makosa yanayochunguzwa yanaweza kuwa na adhabu ya hadi miaka 30 jela. Puigdemont, alisema yeye pamoja na wajumbe wengine walikimbilia Ubelgiji kwa ajili ya "uhuru na usalama". Waliokuwa mawaziri wawili walirejea Uhispania na wanatarajiwa pia kuwa miongoni mwa wabunge 15 wanaotarajiwa kujitokeza mahakamani.

Wanasiasa kadhaa na maafisa wengine waliochaguliwa kutoka vyama vya wanaotaka kujitenga katika jimbo hilo wamekusanyika nje ya mahakama kuwaunga mkono wenzao.

Spanien Mariano Rajoy und  Soraya Saenz de Santamaria
Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy na makamu wake Soraya Saenz de SantamariaPicha: Reuters/S. Vera

Waziri Mkuu Mariano Rajoy alimfuta kazi Puigdemont na serikali yake siku ya ijumma, masaa machache baada ya bunge la Catalonia kutoa tangazo la upande mmoja la kujipatia uhuru, kura ambayo iligomewa na upinzani na kutangazwa kuwa si halali na mahakama za Uhispania. Mkazi mmoja wa Barcelona Paul Gil anazungumzia hatua ya Puigdemont kukimbia nchini.

Puigdemont na timu yake ya zamani waliitwa na mahakama kuu wakati spika wa bunge na wabunge wengine waliitwa na mahakama ya juu. Wataamua pia ikiwa wale walioitwa kutoa ushahidi wakae jela wakati uchunguzi ukiendelea. Uwezekano mwingine ni kupataiwa dhamana ya masharti au kuwaamuru kusalimisha pasipoti zao. Mahakama tayari imewaeleza viongozi hao waliotaka kujitenga kuweka kiasi cha euro milioni 6.2 kufikia Ijumaa ili kufidia madeni.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman