1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kumbukumbu ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia

4 Novemba 2018

Ufaransa inaandaa kumbukumbuku za wiki nzima za Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kuanzia Jumapili 04.11.2018, ambapo viongozi 80 kutoka kote ulimwenguni watashiriki maadhimisho ya karne moja tangu vita hivyo vilipokamilika

https://p.dw.com/p/37d5H
Frankreich Tag des Waffenstillstands
Picha: picture-alliance/abaca/C. Liewig

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anajiandaa kwa wiki yenye shughuli nyingi za kidiplomasia ambapo atakuwa mwenyeji wa viongozi akiwemo Rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa Urusi Vladmir Putin.

Pia atafanya ziara za Kaskazini mwa Ufaransa, akitembelea maeneo yaliyohushudia mapambano ambako mamia kwa maelfu ya wanajeshi walipoteza maisha yao kwenye mitaro.

Atatumia fursa hiyo ya kimataifa kutoa onyo dhidi ya kuongezeka kwa siasa kali za umaarufu – mbele ya Trump anayendeleza sera ya "Marekani Kwanza" na viongozi wengine wa siasa za kizalendo.

Maadhimisho hayo yatafikia kilele chake katika sherehe itakayofanyika katika lango la Arc de Triomphe mjini Paris, Novemba 11 na kuhudhuriwa na viongozi kadhaa akiwemo Trump, Putin na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, miaka 100 tangu kusainiwa makubaliano ya kuweka chini silaha.

Frankreich Gedenktag Ende des Zweiten Weltkrieges in Europa
Macron akiweka shada la maua kwenye mnara wa kaburi la mwanajeshi asiyejulikana mjini ParisPicha: Reuters/F. Guilllot

Hafla katika eneo la mnara wa Kaburi la Mwanajeshi Asiyejulikana kwenye mtaa wa Champs-Elysees itafanyika chini ya ulinzi mklai kufuatia msururu wa mashambulizi makali ya wanamgambo wa itikadi kali nchini Ufaransa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Matukio ya kumbukumbu yataanza Jumapili, Novemba 4, kwa tamasha la muziki linaloadhimisha urafiki kati ya maadui wawili wa zamani wakati wa vita Ufaransa na Ujerumani katika mji wa mpakani wa Strasbourg, litakalohudhuriwa na Macron na Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier.

Macron atatumia wiki nzima kuyatembelea maeneo yaliyoshuhudia mapambano katika upande wa Magharibi, kutoka Verdun hadi Somme.

Siku ya Jumanne, katika heshima ya "wanajeshi weusi” wa vikosi vya makoloni ya zamani vilivyopigana pamoja na jeshi la Ufaransa, yeye na Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita watazuru Reims, mji uliolindwa na wanajeshi wa Kiafrika.

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May ataungana na Macron katika eneo la mto Somme siku ya Ijumaa, wakati Jumamosi  Rais huyo wa Ufaransa ataelekea pamoja na Merkel katika kijiji cha Rethondes, ambako saini ya kusitisha vita iliwekwa.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP