Viongozi wa G7 waanza kuwasili Japan kwa mkutano wa kilele
18 Mei 2023Viongozi wa nchi saba tajiri na zilizoendelea zaidi ulimwenguni, wameanza kuwasili mjini Hiroshima nchini Japan kwa mkutano wa kilele.
Kwenye mkutano huo wa siku tatu, viongozi hao wa kundi la G7, wanatarajiwa kujadili masuala kadha wa kadha, huku vita vya Urusi nchini Ukraine, vikitarajiwa kutawala mazungumzo yao.
Serikali ya Marekani imedokeza uwezekano wa suala la vikwazo vipya dhidi ya Urusi kujadiliwa kwenye mkutano wa kilele wa Hiroshima.
Mwenyeji wa mkutano huo, Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida amefanya mazungumzo ya pembeni na mwenzake wa Italia Giorgia Meloni na kusema:
"Tumekubaliana kuimarisha ushirikiano wetu wa kimkakati kati ya Japan na Italia na ningependa kuendelea na ushirikiano huo huko baadae ."
Kundi la G7 linajumuisha Marekani, Uingereza Ujerumani, Ufaransa, Italia, Canada, Japan na vilevile Umoja wa Ulaya.