Viongozi duniani walaani shambulio la Kabul
31 Mei 2017Viongozi mbalimbali duniani wamelaani vikali shambulizi la bomu lilotokea mapema leo mjini Kabul nchini Afghanistan katika eneo la balozi mbalimbali na majengo muhimu ya serikali. Idadi ya waliofariki kufutia shmabulizi hilo imeongezeka na kufikia watu 80 na wengine 350 kujeruhiwa.Bomu hilo lilikuwa limetegwa kwenye gari.Akizungumza katika mji wa Nuremberg hapa Ujerumani kansela Angela Merkel amesema shambulizi hilo ni ishara kuwa ugaidi hauna mipaka. Polisi imethibitisha kuwa mlipuko huo ulitokea karibu sana na ubalozi wa Ujerumani,na wafanyakazi kadhaa wa ubalozi huo ni miongoni mwa waliojeruhiwa.Merkel amesema vita dhidi ya ugaidi vitaendelea.Sote kwa pamoja, tunaoamini haki,Uhuru na hadhi ya binadamu barani ulaya, Marekani, Afrika pamoja na Afghanistan tutaendelea na mapambano dhidi ya magaidi na tutashinda.China ,Ufaransa na Uturuki zimesema hakuna mfanyakazi wake hata mmoja alijeruhiwa kufuatia shambulio hilo ambapo idadi kubwa ya waliofariki ni raia wa Afghanistan.Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema wameanza kuwaondoa raia wake mji Kabul baada ya kuharibiwa vibaya ubalozi wake.Waziri huyo ametaka uchunguzi kamili ufanyike kuhusu jinsi gari hilo lilokuwa na bomu lilivyoweza kufika mjini Kabul ambako kuna ulinzi mkali kutokana na kuwa na makaazi ya wanadiplomasia."Nimekuwepo kwenye mji huo mara nyingi .Hili ni shambulizi baya.Sielewi vipi gari hilo liliweza kupita vizuizi mbalimbali vya polisi.Tumshukuru mungu hakuna mfanyakazi yeyote wa ubalozi wetu aliyejeruhiwa. Tutawatuma wachunguzi wetu nchini Aghanistan kukusanya ripoti kamili kuhusu shambulizi hilo. Lakini kwa mara nyingine tunalaani shmabulizi hilo la kigaidi na tutaendelea kuwasaidia ndugu zetu Waafghanistan."Ubalozi wa Marekani mjini Kabul na ujumbe wa jumuiya ya Nato nchini humo umelaani vikali shambulizi hilo ambalo limetajwa kuwa baya zaidi tangu kuondoka majeshi ya kigeni nchini humo mwishoni mwaka 2014. Hadi sasa haifahamiki kwanini shambulizi hilo lililenga eneo la Wazir Akbar Khan, na hakuna kundi lilojitokeza kudai kuhusika ingawa wapiganaji wa Taliban na wale wa IS wamekuwa wakiwahangaisha raia hasa katika mji huo wa Kabul. Vikosi vya Marekani na vile vya Afghanistan vimekuwa vikakabiliana na uasi wa kundi la Taliban kwa zaidi ya miaka 15. Marekani kwasasa ina zaidi ya majeshi elfu 8 nchini humo,na imekuwa ikitoa mafunzo kwa wanajeshi wa Afghanistan na pia kuhusika na operesheni za kukabiliana na magaidi.
Mwandishi:Jane Nyingi
Mhariri:Yusuf Saumu