1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi duniani wakaribisha mpango wa kunusuru masoko yake ya fedha

Mohmed Dahman4 Oktoba 2008

Viongozi wa mataifa makubwa ya kiuchumi duniani leo wamekaribisha kuidhinishwa na wabunge wa Marekani kwa mpango wa dola bilioni 700 kuokowa masoko yake fedha na kuita hatua hiyo kuwa ya uwajibikaji na yenye kuhitajika.

https://p.dw.com/p/FU4j
Rais George W. Bush wa Marekani amesaini muswada wa mpango wa kuokowa masoko ya fedha ya nchi.Picha: AP

Waziri wa uchumi wa Ufaransa Christine Lagarde amesema yuko furahani sana na kwamba hatua hiyo ilikuwa inahitajika kuchukuliwa.

Waziri Mkuu wa Australia Kevin Rudd ameikaribisha hatua hiyo kwa kusema kwamba bado hatua zaidi zinahitajika kuchukuliwa kukabiliana na mgogoro huo wa fedha.

Ruud anasema hilo limekuwa zoezi gumu kwa Marekani lakini ukiangalia kupindukia hatua hiyo hivi sasa wanakabiliwa na changamoto juu ya kuwepo kwa taratibu za fedha aza kuaminika duniani na kwamba jambo hilo ni muhimu sana katika kurudisha utulivu wa kutoyumba kwa mfumo wa mabenki na fedha duniani kwa kipindi cha muda mrefu na pia ni muhimu katika kurudisha imani katika mfumo wa mabenki.

Mjini Brussels Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya Emmanuel Barroso amesema wabunge wa Marekani wameonyesha kuwajibika katika kuushughulikia mgogoro huo wa fedha uliosababishwa kwa kiasi kikubwa na mikopo mibaya ya nyumba ya Marekani.

Rais George W. Bush wa Marekani amesaini muswada wa mpango huo kuwa sheria na Waziri wa Fedha wa Marekani Henry Paulson ameahidi kuchukuwa hatua haraka kutekeleza mpango huo ikiwa ni hatua kubwa kabisa ya serikali kuingilia kati hali ya uchumi kuwahi kushuhudiwa nchini humo tokea kuathirika vibaya sana kwa uchumi katika miaka ya 1930.