1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi Afrika Mashariki wahimiza mazungumzo haraka Sudan kusini

28 Desemba 2013

Viongozi wa Afrika mashariki Ijumaa (27.12.2013) wamemtaka rais wa Sudan kusini Kiir na hasimu wake kisiasa Machar kukutana ana kwa ana katika muda wa siku nne kumaliza ghasia zinazoongezeka katika taifa hilo changa.

https://p.dw.com/p/1Ahnp
IGAD Treffen Nairobi
Mkutano wa IGAD , NairobiPicha: picture-alliance/dpa

Viongozi hao wamemtaka rais Kiir na makamu wake wa zamani Machar kukutana kabla ya mwisho wa mwaka huu, na kuongeza kuwa hawatakubali serikali ya Sudan kusini kuangushwa kwa kutumia jeshi.

"Iwapo uhasama hautamalizika katika muda wa siku nne, mkutano huo utafikiria hatua zaidi za kuchukua," Waziri wa mambo ya kigeni wa Ethiopia Tedros Adhanom amewaambia waandishi habari mwishoni mwa mkutano wao mjini Nairobi.

Südsudans Präsident Salva Kiir und Kenias Präsident Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta (kulia) na Salva Kiir (shoto)Picha: Reuters

Kiir alikutana na rais Uhuru Kenyatta wa Kenya siku ya Alhamis katika mji mkuu wa sudan kusini Juba.

Machar atuma ujumbe wa ukaidi

Lakini Machar alituma ujumbe akionesha hali ya upinzani kupitia shirika la habari la BBC siku ya Ijumaa akiwa msituni, akitangaza kuwa masharti ya kusitisha mapigano hayajatekelezwa. Amedokeza kuwa washirika wake wawili tu wa kisiasa ndio ambao wameachwa huru kutoka kifungoni miongoni mwa kumi na mmoja ambao anataka waachiwe huru.

Südsudan Riek Machar Vize-Präsident ARCHIVBILD
Makamu wa rais wa zamani wa Sudan kusini Riek MacharPicha: Getty Images/AFP

Wafungwa hao wanashtakiwa kwa kujaribu kufanya mapinduzi kumwangusha rais Kiir kutoka madarakani. Mapigano , ambayo yalizuka Desemba 15 katika mji mkuu Juba na kusambaa haraka hadi katika majimbo sita kati ya kumi nchini humo, yanaripotiwa yamesababisha mamia kwa maelfu ya watu kupoteza maisha na mamia kwa maelfu wamekimbia makaazi yao.

Viongozi wa nchi kutoka Kenya, Uganda, Ethiopia, Somalia na Djobouti walikutana na waziri wa mambo ya kigeni wa Sudan kusini pamoja na makamu wa rais wa Sudan.

Mkutano "unashauri hatua za haraka kutoka pande zote kuanza mazungumzo," ukihimiza "utafutaji wa haraka wa suluhisho la kisiasa," viongozi hao wamesema katika taarifa.

Präsident Salva Kiir Südsudan Süd Sudan Porträt
Rais wa Sudan kusini Salva KiirPicha: Reuters

Pia "wamekaribisha nia ya serikali ya jamhuri ya Sudan kusini ya kusitisha mapigano mara moja na kumtaka Dr. Riek Machar pamoja na wadau wengine kutoa ahadi kama hizo."

Machar bado yuko mafichoni

Kiir na makamu wake wa zamani Machar , ambae majeshi yake ya waasi yalianza mzozo huo, hawakuhudhuria mazungumzo hayo.

Machar , ambaye yuko mafichoni , anadai kuwa kiir ajiuzulu. Amemshutumu rais kuwa ni dikteta , wakati Kiir ameeleza nia yake ya kutaka kufanya majadiliano ya kumaliza mapigano na kuingia katika mazungumzo bila masharti.

Südsudan - UN
Wanajeshi wa jeshi la kulinda amani la UM nchini Sudan kusiniPicha: Reuters

Viongozi hao walikuwa wanakutana kama sehemu ya mkutano maalum wa mamlaka ya serikali za pamoja kuhusu maendeleo IGAD, siku moja baada ya mazungumzo ya pande tatu katika mji wa Juba nchini Sudan kusini kati ya rais Kiir, Kenyatta na waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Sesalegn.

Wakati huo huo kundi la kwanza la wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani wamewasili Sudan kusini, siku tatu baada ya baraza la Usalama la Umoja wa mataifa kuongeza mara mbili idadi ya jeshi la kulinda amani katika nchi hiyo ya Afrika mashariki. Vikosi vipya vilivyowasili ni polisi 72 kutoka Bangladesh. Vikosi vya ziada vitakuwa na jumla ya wanajeshi 5,500, pamoja na polisi 440, ambao wameidhinishwa rasmi siku ya Alhamis.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae /

Mhariri: Sudi Mnette