1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vinyago vilivyochukuliwa wakati wa Ukoloni virejeshwe Afrika

Oumilkheir Hamidou
30 Novemba 2018

Vinyago vyaAfrika,, matumizi ya nguvu ya Boko Haram nchini Nigeria na mzozo kati ya wachimba dhahabu na wanajeshi wa Tchad katika milima ya Tibesti ni miongoni mwa yaliyomo katika Afrika katika magazeti ya Ujerumani

https://p.dw.com/p/39Ci7
Cartoon - Buhari fighting Boko Haram
Picha: DW

Magazeti mashuhuri ya Ujerumani yamejishughulisha na uamuzi wa rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wa kurejeshwa vinyago vyote vinavyopamba majengo ya makumbusho na taasisi nyengine za nchi hiyo na ambavyo vilichukuliwa  wakati wa ukoloni wa Ufarasa barani Afrika."Sawa, si sawa, uamuzi wa pupa, hauna maana , au wa kijasiri "ndio kichwa cha maneno cha gazeti la Süddeutsche Zeitung kuhusu  kurejeshwa nchini Benin vinyago 26 viliovyochukuliwa mwaka 1892 na jenerali Dodds na ambavyo tangu wakati huo  viongozi wamekuwa wakidai virejeshwe.

Uamuzi wa rais Emmanuel Macron, linaandika gazeti la Süddeutsche unafuatia ripoti iliyoandaliwa na wataalam wawili wa kifaransa Bénédicte Savoy na Felwine Sarr kuhusu  vinanyango hivyo. Majibu tofauti yamejitokeza ; Katika wakati ambapo rais wa Ufaransa anataka virejeshwe , miongoni mwa wananchi na viongozi wa majengo ya makumbusho misimamo yao inatofautiana pia kati ya wale wanaouona uamuzi huo  kuwa unastahiki sifa na wale wanaoukosoa.

Vinyago vimechukuliwa vipi?

Mkurugenzi mkuu wa jengo la makumbusho la jijini Paris Musée du Quai-Branly, Stephane Martin alikuwa mmojawapo wa wale waliounga mkono hapo awali juhudi za kutaka vinyago vya nchi za Afrika virejeshwe. Lakini uamuzi wa rais Macron umemshangaza. Gazeti linajiuliza makumbusho hayo yatakuwa ya aina gani watakapolazimika kurejesha vinyago 46000-vinyago vingi zaidi kupita jengo lolote jengine nchini Ufaransa?

Frankfurter Allgemeine pia limezungumzia kadhia hiyo. Kichwa cha maneno "Nani anajihisi kaibiwa". Linawanukuu waasisi wa ripoti inayotaka warejeshewe wenyewe waafrika, wakisema vinyago hivyo vimechukuliwa kinyume na sheria wakati wa enzi za ukoloni. Frakfurter Allgemeine linajiuliza sheria gani zilitumiwa mwaka 1884,1904 au hata mwaka 1915 na watawala wa kikoloni wa kijerumani zama hizo? Na kama vinyago vilivyochukuliwa vilitolewa kama zawadi au kutokana na shinikizo, au vilinyakuliwa. Masuala hayo hadi sasa, linasema Frankfurter Allgemeine, yamekuwa yakijadiliwa kwa kuzingatia mtazamo wa kihistoria tu.

Afrika katika Magazeti ya Ujerumani

 Mashambulio ya kikatili ya Boko Haram nchini Nigeria

Lilikuwa gazeti hilo hilo la mjini Frankfurt-Frankfurter Allgemeine lililoandika kuhusu kuzidi matumizi ya nguvu ya kundi la itikadi kali la Boko Haram nchini Nigeria. Gazeti linazungumzia shambulio la kikatili kabisa kuwahi kushuhudiwa nchini NIgeria tangu rais Muhammadu Buhari alipokabidhiwa hatamu za uongozi mwaka 2015. Katika kipindi cha wiki moja tu wanamgambo hao wa dola la kiislam katika taifa hilo tajiri kwa mafuta Afrika magharibi, wamewauwa watu 118, zaidi ya 100 kati yao ni wanajeshi. Wamejitambulisha na mauwaji hayo kupitia kanda ya video ya kundi linalojiita "Dola la kiislam katika Afrika Magharibi."

Frankfurter Allgemeine linasema wimbi la mashambulio limeanza Novemba 16 ambapo wanajeshi watatu wameuwawa na wengine kadhaa kutojulikana waliko. Muda mfupi baadae wakawauwa wanawake saba katika mji wa Bama na katika kijiji cha Mammanti wakamuuwa mtu moja na kuiba ng'ombe mia kadhaa. Hujuma za jeshi la wanaanga la Nigeria ndizo zilizosaidia kukomeshwa mashambulio ya wanamgambo hao.

 Kitisho cha kuzuka vita katika milima ya Tibesti

Mada ya mwisho katika ukurasa wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii inatupeleka katika jangwa la Sahara ambako gazeti la die tageszeietung la mjini Berlin linazungumzia kuhusu  mzozo kati ya wachimba dhahabu na wanajesjhi wa Tchad katika milima ya Tibesti. die tageszeitung linasema mzozo huo unachukua sura ya vita na kutishia kuenea pia katika nchi jirani za Libya na Niger. Mzozo huo linaandika gazeti la die tageszeitung unatishia kuwaingiza mpaka wanajeshi wa nchi za magharibi wanaopambana na makundi ya magaidi katika eneo hilo.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/ BASIS/PRESSER/ALL/PRESSE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman