VILNIUS. Russia na Marekani zatofautiana kuhusu Belarus katika mkutano wa NATO.
21 Aprili 2005Russia na Marekani zimetofautiana kuhusu swala la Belarus katika mkutano wa mawaziri wa kigeni wa mataifa wanachama wa shirika la NATO unaofanyika mjini Vilnius nchini Lithunia. Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, ameitaja Belarus kama taifa la pekee katika Ulaya ya kati linaloendeleza maongozi ya kidikteta. Amesema rais Lukaschenko ni dikteta mkubwa barani Ulaya, na akasisitiza kwamba wakati umewadia mageuzi yafanyike nchini Belarus.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Russia, Silvio Lavrov, akiyajibu matamshi hayo ya Rice, alisema Russia haiwezi kukubali kile watu wanachokiita mabadiliko ya maongozi. Baada ya matamshi hayo ya Lavrov, Condoleezze Rice alikutana mara moja na viongozi wa upinzani wa Belarus wanaounga mkono demokrasia nchini humo, licha ya Russia kuelezea wasiwasi wake kwamba Marekani inayaingilia mataifa yaliyokuwa chini ya utawala wake zamani.
Wakati huo huo, NATO imesaini mkataba na Russia, hivyo kuboresha uhusiano na taifa hilo. Mawaziri wameapa kwa kauli moja kuisaidia Ukraine kuendeleza mageuzi ya kuelekea mataifa ya magharibi, kufuatia mapinduzi ya manjano yaliyohatarisha uhusiano na serikali ya Moscow.