1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Marekeni kuondoka Afghanistan 2014 huku jina la mwanajeshi aliyeuwa raia 16 huko lafichuliwa

MjahidA17 Machi 2012

Rais wa Marekani Barrack Obama na mwenzake wa Afghanistan Hamid Karzai wamethibitisha kwamba majeshi ya Marekani yataondoka nchini humo mwishoni mwa mwaka 2014.

https://p.dw.com/p/14Lzp
Rais Barrack Obama wa Marekani na mwenzake wa Afghanistan Hamid Karzai
Rais Barrack Obama wa Marekani na mwenzake wa Afghanistan Hamid KarzaiPicha: picture-alliance/dpa

Hatua hii imechukuliwa licha ya miito ya kutaka jeshi la Marekani kuondolewa nchini humo mapema. Marais hao ambao waliozungumza kwa njia ya simu walisisitiza kwamba wataendelea na utekelezaji wa utaratibu wa Lisbon ambapo majeshi ya Afghanistan yatakamilisha hatua za mpito na kuchukua jukumu la usalama nchini humo ifikapo mwishoni mwa mwaka 2014.

Awali rais Hamid Karzai wa Afghanistan alikuwa na shaka iwapo mauaji yalitekelezwa na mtu mmoja. Karzai amesema mtu mmoja hawezi kuingia katika nyumba ya familia moja ndani ya vyumba vinne na kuwauwa wanawake na watoto, kisha wote akawaleta katika chumba kimoja na kuwachoma moto.

Uchunguzi wa pamoja unafanywa na Marekani na Afghanistan, kubaini kilichopelekea mwanajeshi huyo kuwauwa raia hao 16. Iwapo itabainika kwamba sio mwanajeshi mmoja aliyetekeleza kisa hicho basi hii itakuwa pigo kubwa kwa jeshi la Nato.

Jina la Mwanajeshi lafichuliwa

Huku hayo yakiarifiwa, afisa mmoja nchini Marekani amesema Robert Bales mwenye umri wa miaka 38 ndiye mwanajeshi anayeshutumiwa kwa mauaji ya raia 16 wa Afghanistan. Robert Bales ameoa na ana watoto wawili.

Afisa huyo aliyezungumza bila kutaka kutajwa jina lake alikataa kutoa maelezo zaidi juu ya mwanajeshi huyo anayeaminika kutoka katika kambi ya jeshi la Marekani nchini Afghanistan siku ya Jumapili na kutekeleza mauaji ya raia hao 16.

Waandamanaji nchini Afghanistan
Waandamanaji nchini AfghanistanPicha: Reuters

Hali hii imezua wasiwasi katika mahusiano kati ya Marekani na Afghanistan, hususan baada ya kisa cha hapo awali cha wanajeshi wa Marekani kuchoma kitabu kitakatifu cha waumini wa Kiislamu.

Kulingana na jeshi la Marekani, Mwanajeshi huyo Robert Bales aliwasili siku ya Ijumaa katika kambi ya jeshi nchini Marekani , katika eneo la Kansas,anakozuiliwa katika jela moja kabla ya kufunguliwa mashtaka.Bales alikuwa Iraq kabla ya kupelekwa Afghanistan.

Hata hivyo hadi sasa bado jeshi la Marekani haijatoa rasmi jina la mwanajeshi huyo wala kumfungulia mashtaka yoyote. Wachunguzi wa jeshi wanajaribu kupata maelezo zaidi juu ya kisa hiki.

Mwandishi: Amina Abubakar/RTRE

Mhariri Sekione Kitojo