1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Maduro vyazuwia misafara ya msaada mpakani

24 Februari 2019

Vikosi tiifu kwa Rais Nicolas Maduro vimezuwia malori ya msaada kuingia Venezuela Jumamosi kwa kutumia gesi ya kutoa machozi na risasi, na kuuwa waandamanaji wawili, na kuweka uwezekano wa makabiliano na Washington.

https://p.dw.com/p/3Dz6Q
Kolumbien Hilfslieferungen für Venezuela
Picha: picture alliance/AP Photo/F. Vergara

Malori yaliyojazwa chakula na dawa kutoka Marekani kwa ajili ya Venezuela yalirejea kwenye maghala nchini Colombia baada ya wafuasi wa upinzani kushindwa kuvunja vizuwizi vya wanajeshi, na kusababisha waandamanaji kadhaa kujeruhiwa. Mashuhuda walisema askari kanzu waliofunika nyuso zao pia waliwafyatulia risasi za moto waandamanaji.

Baada ya kukasirishwa na uungwaji mkono wa serikali ya Colombia kwa kiongozi wa upinzani Juan Guaido, Maduro alisema alikuwa anavunja uhusiano wa kidiplomasia na serikali mjini Bogota na kuwapa wafanyakazi wa ubalozi masaa 24 kuondoka nchini humo.

Guaido, ambaye mataifa mengi ya Magharibi yanamtambua kama kiongozi halali wa Venezuela, alizindua msafara huo wa msaada kutoka mji wa Cucuta nchini Colombia siku ya Jumamosi.

Upinzani ulitaraji kwamba wanajeshi wa Venezuela wangesita kurudisha misaada hiyo inayohitajika vibaya nchini humo, ambako idadi inayoongezeka ya raia wake milioni 30 wanakabiliwa na tatizo la utapiamlo na magonjwa yanayotibika.

Lakini licha ya wanachama 60 wa vikosi vya usalama waliasi siku ya Jumamosi, kwa mujibu wa maafisa wa Colombia, vikosi vya ulinzi wa taifa vilisalia imara kwenye maeneo ya mpakani, vikiifyatulia gesi ya kutoa machozi misafara hiyo.

Kolumbien Hilfslieferungen für Venezuela
Juan Guaido akiwapa dole wafuasi wake katika mji wa mpakani wa Cucute pembeni mwa lori lililobeba msaada Februari 23.2019Picha: Getty Images/AFP/G. Munoz

Kwenye kituo cha mpakani cha Urena, malori mawili ya misaada yalishika moto na kusababisha moshi mzito angani huku makundi ya watu yakikimbia kujaribu kunusuru maksha ya ugavi, alisema shuhuda wa shirika la habari la Reuters.

Guaido, akizungumza baadae kutokea Colombia, alisema ataendelea kumshinikiza Maduro aruhusu msaada uingie nchini na kwamba atatafuta njia nyingine. Alisema atahudhuria mkutano wa kundi la mataifa ya kikanda la Lima mjini Bogota siku ya Jumatatu pamoja na makamo wa rais wa Marekani Mike Pence.

"Leo dunia imeona katika muda wa dakika, saa, sura mbaya zaidi ya udikteta wa Venezuela," alisema Guaido akiwa pamoja na rais wa Colombia Ivan Duque. "Tumemuona mwanaume asiyehisi maumivu ya watu wa Venezuela, alieamuru kuchomwa kwa chakula muhimu kwa watu walio na njaa."

Maduro anakanusha kuwa nchi yake yenye utajiri wa mafuta ina uhitaji wowote wa msaada na anamtuhumu Guaido kwa kuwa mchochezi wa mapinduzi na kibaraka wa Rais wa Marekani Donald Trump. Washington imeonya kuwa inaweza kuweka vikwazo vipya vikali zaidi dhidi ya Venezuela wakati wa mkutano wa Jumatatu iwapo Maduro ataendelea kuzuwia uingizwaji wa misaada.

"Watu wa Venezuela wanafikiria nini kuhusu vitisho vya Donald Trump? Achana na Venezuela. Yankee nenda nyumbani," Maduro aliuambia mkutano wa hadhara uliohufhuriwa na wafuasi wake waliovalia fulana nyenkundu katika mji mkuu Caracas. "Anatutumia chakula kilichooza, ahsante!"

Mshauri wa usalama wa taifa wa Trump John Bolton alisema kupitia ukurasa wa twitter kwamba mataifa yanayoendelea kumuunga mkono Maduro "yanapaswa kuzingatia wanachokiidhinisha", katika karipio lisilo la dhahiri dhidi ya China na Urusi.

Venezuela San Antonio del Tachira Maduro-Paramilitärs bedrohen Opposition
Wanamgambo wanaoiunga mkono serikali wakitumia bastola kuwatawanya waandamanaji.Picha: Getty Images/AFP/F. Parra

'Uhuru'

Katika miji ya mpakani ya Venezuelea ya San Antonio na Urena, vikosi viliwafyatulia risasi za mpira wafuasi wa upinzani wakiwemo wabunge, waliotembea kuelekea mpaka wakipunga bendera za Venezuela na kuimba "uhuru".

Picha ya televisheni za Reuters kutoka San Antonio zilionyesha wanaume kadhaa wakiwa kwenye pikipiki, wakiwa wamevalia mavazi meusi na kufunika vichwa vyao, wakifyatua bunduki na bastola kwenye kundi la watu.

Waandamanaji mjini Urena walizuwia mitaa kwa mataifa ya moto, wakalichoma moto basi na kuwarushia mawe wanajeshi wakitaka Maduro aruhusu msaada uingie katika taifa ambalo limevurugwa na mgogoro uliopunguza uchumi wa kwa nusu katika kipindi cha miaka mitano.

"Walianza kufyatua risasi kwa ukaribu kana kwamba tulikuwa wahalifu," alisema muuza duka Vladmir Gomez, 27, aliekuwa amevalia shati jeupe leyne damu. Magari yasiopungua sita yaliojaribu kuingia Venezuela yalirejea Cucuta baadae, ambako wakala wa usimamizi wa majanga wa Colombia ulisema yangepakuliwa na misaada kuhifadhiwa tena hadi Guaido aombe tena matumizi yake.

Gavana wa jimbo la Perto Rico Ricardo Rossello alisema ameiamuru meli ya Puerto Rico iliobeba msada ya kibinadamu kurudi baada ya meli ya jeshi la Venezuela kutishia kuishambulia. "Hii haikubaliki na ni aibu," Rossello alisema katika taarifa. "Tumewaarifu pia washirika wetu katika serikali ya Marekani kuhusu tukio hili zito."

Venezuela Grenzstadt Ureña Proteste
Wavenezuela wakiwakabili askari polisi wakiwataka waruhusu misaada iingizwe nchini.Picha: AFP/J. Barreto

Kwa mujibu wa shuhuda wa shirika la habari la Reuters, malori mawili ya msaada yalivuka mpaka wa Brazil lakini hayakupita kituo cha ukaguzi wa forsha cha Venezuela. Katika mji wa kusini wa Santa Elena de Uairen watu wasiopungua wawili waliuawa katika makabiliano na vikosi vya usalama, kulingana na daktari wa hospitali walikotibiwa.

Kundi la kutetea haki la Penal Forum lilisema limerikodi majeruhi 29 kutokana na risasi na vifo viwili nchini Venezuela katika makabiliano na wanajeshi siku ya Jumamosi. Maafisa wa Colombia walisema wamesajili majeruhi 285, wakiwemo walioathirika na gesi ya kutoa machozi, alisema waziri wa mambo ya nje Carlos Holmes Trujillo.

Dazeni kadhaa waasi

Guaido alivitolea mwito vikosi vya ulinzi na usalama vya Venezuela kusimama kando na kuruhusu msaada uingie, akiahidi msamaha kwa maafisa wote wanaojitenga na Maduro. Wanajeshi kadhaa, ambao familia zao zinakabiliwa na uhaba sawa kama Wavenezuela wengine, waliitikia wito wake.

"Huwezi kumtii mtu ambae anasherehekea kwa kejeli kwamba msaada wa kiutu hauingii katika taifa linalouhitaji," alisema Guaido siku ya Jumamosi. Mkanda wa vidio wa mitandao wa kijamii ulionyesha wanajeshi walioacha vituo vyao kwenye daraja linaloiunganisha Venezuela na Colombia, wakaondoa vizuwizi vya chuma na kisha kuruka kutoka  kwenye magari yao na kukimbilia upande wa Colombia.

Venezuela | Konzert an der Grenze zu Kolumbien in Urena
Watu wakitoa ishara wakati wa tamasha la siku tatu la kiunga mkono serikali lililoitishwa na rias Maduro.Picha: Getty Images/AFP/J. Barreto

"Tulichofanya leo, tulifanya kwa ajili ya familia zetu, kwa ajili ya watu wa Venezuela," alisema mmoja wa watoro hao katika ukanda wa video uliorushwa kwenye kipindi cha habari cha televisheni ya Colombia.

Chama tawala cha Kisoshalisti nchini Venezuelea kinazitaja juhudi za misaada za Guaido kuwa uvamizi uliojificha unaoungwa mkono na Marekani na kinasisitiza kwamba Marekani inapaswa badala yake kuisaidia Venezuela kwa kuondoa vikwazo vinavyolemaza sekta za kifedha na mafuta.

Siku ya Jumamosi, Maduro aligeuza hasira zake kwa Colombia na kusema rais Duque ameacha ardhi yake itumiwe kwa mashambulizi dhidi ya Venezuela. "Kwa sababu hiyo, nimeamua kuvunja uhusiano wote wa kisiasa na kidiplomasia na serikali ya kifashisti ya Colombia," aliwambia wafuasi wake waliokuwa wakishangilia.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre

Mhariri: Zainab Aziz