1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Israel lawauwa Wapalestina 4 Ukingo wa Magharibi

6 Agosti 2024

Jeshi la Israel limewauwa watu wanne mjini Jenin katika Ukingo wa Magharibi linaoukalia kimaubavu. Hayo ni kwa mujibu wa maafisa wa afya katika eneo hilo.

https://p.dw.com/p/4j9h9
Mwanamume akiwa na bendera ya Palestina eneo la Ukingo wa Magharibi
Mwanamume akiwa na bendera ya Palestina eneo la Ukingo wa MagharibiPicha: Jaafar Ashitiyeh/AFP via Getty Images

Vifo hivyo vimefuatia usiku wa machafuko ambapo watu wengine wanne waliuawa katika makabiliano karibu na eneo la Tubas, karibu na mpaka na Jordan.

Jeshi la Israel limesema lilifanya mashambulizi mawili tofauti ya angani katika Ukingo wa Magharibi, likidai kuwauwa wanamgambo, bila kutoa maelezo zaidi.

Shirika la Hilal Nyekunde la Kipalestina limethibitisha kuwa watu wanne waliuawa katika mashambulizi hayo yaliyoyalenga magari mawili mjini Jenin, mojawapo ya maeneo tete zaidi katika Ukingo wa Magharibi.  

Soma pia:Wapalestina watano wauawa kwa droni katika Ukingo wa Magharibi

Wakati huo huo, Iran imetetea haki yake ya kuiadhibu Israel, kwa mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa kundi la Hamas, Ismail Haniyeh, mjini Tehran, wiki iliyopita.

Hata hivyo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kanaani, amesema Iran haitaki kuendeleza mzozo wa kikanda katika Mashariki ya Kati, lakini ina haki kisheria kuiadhibu Israel.