1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Gadhafi vimeirejesha miji yenye nafuta

Admin.WagnerD30 Machi 2011

Vikosi vinavyomtii kiongozi wa Libya Muammar Gadhafi,vimefanikiwa kuwarudisha nyuma waasi na kuyashikilia maeneo kadhaa yenye hazina ya mafuta kama Ras Lanuf, Es Sider na vinaelekea katika mji wa Brega.

https://p.dw.com/p/10ktS
Vikosi vinavyomtii Kanali Muammar GadhafiPicha: AP

Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Uingereza-Reuters,idadi kubwa ya Waasi wakiwa na zana za kivita hivi sasa wanarudi nyuma katika mji mwingine wa Ajdabiyah.

Mmoja kati ya waasi Mohamed al-Abreigi alisema"tunakwenda Ajdabiyah na Mungu akijalia leo tutarudi tena Brega". haijaweza kufahamika ikiwa wanajeshi wa Gaddafi wameuuteka mji huo au la.

Al-Abreigi alisema ndege za kivita zilivishambulia vikosi vya Gadhafi muda mfupi baada yao kuondoka eneo hilo.

Katika tukio lingine watu 18 wameuawa baada ya vikosi vya hivyo vinavyomtii, Muammar Gadhafi kufanya mashambulizi mengine mjini Misrata.

Tukio hilo limetajwa kusababisha vifo vya watu hao 18,wakiwemo wanne wa familia moja,hata hivyo awali taarifa za serikali ya nchi hiyo ilisema imesitisha mapigano katika mji huo baada ya kudai umeudhibiti,ambapo pia karibu watu 200 wamepoteza maisha tangu tarehe 18 mwezi huu.

Hivi sasa kumezuka mjadala kuhusu kuwapa silaha waasi nchini Libya. Waziri wa masuala ya kigeni wa Urusi, Sergej Lavrov amenukuliwa akisema "Hivi karibuni Ufaransa kupitia Waziri wake wa Mambo ya Nje,Alain Juppe, ilisema ipo tayari kuzungumza na washirika wake juu ya kuwapa waasi silaha nchini Libya,lakini Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen alipinga hatua hiyo na sisi tunakubaliana na hatua hiyo.

Katika hatua nyingine Uingereza imewafukuza Wanadipromasia watano kwa kitendo chao cha kumuunga mkono Kanali Gadhafi na kuwatisha wapinzani.

Akilieleza Bunge la Uingereza,Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi hiyo,William Hague amesema tayari ameagiza maafisa hao wakiwemo waambata wa kijeshi, waondokea mara moja kwa kuwa kuwepo kwao nchini humo kutahatarisha hali ya usalama nchini Uingereza.

BRIC Gipfel Hu Jintao
Rais wa China Hu JintaoPicha: AP

Nae Rais wa China Hu Jintao amekosoa mashambulizi ya anga yanayofanya na ndege za kijeshi za majeshi ya muungano dhidi ya vituo vya kijeshi vya vikosi vya Kanali Gadhafi.

Akinukuliwa na chombo kimoja cha habari nchini humo, Hu Jintao akizungumzia Libya na Rais wa Ufaransa,Nicolas Sarkozy amesema mazungumzo na njia nyingine za amani ndio suluhu ya mapigano yanayoendelea sasa.

Rais huyo wa China aliendelea kusisitiza kwamba,historia inaonesha kwamba,utumiaji nguvu katika utatuzi wa migogoro kama hiyo unasbabisha mambo kuwa magumu zaidi.

Nchi hiyo ilionesha mapema msimame wake kuhusu Libya kwa kutaka kusitishwa mashambulizi kwa lengo la kuepusha mauji ya raia wasio na hatia.

Hatua kama hiyo ilichukuliwa vyombo vingine kama Umoja wa nchi za Kiarabu (Arab Leage) na Umoja wa Afrika,kuzuia kutumika nguvu katika ardhi ya Libya.

China,sambamba na Urusi,Brazil,Ujerumani na India zilijizuwia kulipigia kura azimio la umoja wa mataifa liliotaka kuzuia ndege kuruka katika anga yaLibya.Urusi sasa inasema azimio hilo sasa linatumiwa vibaya kwani mashambulizi dhidi ya Libya hayakutajwa katika azimio.

Mwandishi: Sudi Mnette//DPAE/APE/RTRE
Mhariri:Abdul-Rahman