1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikao vya kupima nia ya kuunda serikali ya muungano Berlin

Oumilkheir Hamidou
19 Oktoba 2017

CDU, CSU, FD na walinzi wa mazingira die Grüne wanaonyesha kuridhika na duru ya kwanza ya mazungumzo ya kutathmini uwezekano wa kuunda serikali ya muungano. Pande hizo 4 zimepanga kukutana kwa pamoja ijumaa inayokuja.

https://p.dw.com/p/2m9v8
Deutschland Jamaika-Sondierungen zwischen CDU und Grüne starten
Picha: picture alliance/dpa/B. V. Jutrczenka

Baada ya  wawakilishi wa CDU na CSU kuzungumza na waliberali wa FDP, jioni ikawa zamu ya kukutana na wale wa walinzi wa mazingira die Grüne. Pande zote nne zinaonyesha kuridhika na jinsi mazungumzo hayo yalivyoendelea, kama anavyosema katibu mkuu wa chama cha kansela Angela Merkel Christian Democratic Union CDU, Peter Tauber : "Ikiwa vyama ambavyo misimamo yao ni tofauti-na hilo limebainika katika mazungumzo-vinajaribu kushirikiana, basi hiyo ni ishara muhimu na hasa linapohusika suala la kuondowa kile kinacholeta mtengano katika jamii.Tunabidi hata kusema baada ya duru ya kwanza ya mazungumzo, njia ni ndefu hadi tutakapofikia msimamo wa pamoja. Na ndio maana tunasubiri kwa shauku kubwa duru ya kwanza ya mazungumzo ya pande nne, ijumaa inayokuja."

Kansela Angela Merkel (kushoto) na mkuu wa kundi la wabunge wa walinzi wa mazingira Katrin Göring-Eckerdt (kati)  na mwenyekiti wa chamam hicho Cem Özdemir (kulia)
Kansela Angela Merkel (kushoto) na mkuu wa kundi la wabunge wa walinzi wa mazingira Katrin Göring-Eckerdt (kati) na mwenyekiti wa chamam hicho Cem Özdemir (kulia)Picha: picture alliance/dpa/K. Nietfeld

Sifa zimetolewa pia  na walinzi wa mazingira die Grüne na wahafidhina wa CSU

Na mkuu wa shughuli za chama cha walinzi wa mazingira Michael Kellner amesifu pia mazungumzo hayo akisema wamezungumzia mada na ufumbuzi. Sawa na Tauber na yeye pia amesema njia bado ni ndefu hadi muungano wa vyama vinne unaojitambulisha na rangi nyeusi kwa vyama ndugu vya CDU/CSU, manjano kwa chama cha FDP na kijani kwa walinzi wa mazingira die Grüne, muungano wa Jamaica kama unavyoitwa, utakapoundwa. Na katibu mkuu wa chama cha CSU, Andreas Scheuer amekiri aliposema kampeni za uchaguzi zimeshamalizika,  mazungumzo yalikuwa muhimu na hali  ilikuwa ya kuridhisha, hata hivyo anaongeza kusema mada muhimu zinabidi kujadiliwa.

Nembo ya mazungumzo ya muungano unaoitwa wa Jamaica kati ya CDU/CSU(nyeusi), FDP (Manjano) na walinzi wa mazingira die Grüne wanaojitambulisha na rangi ya kijani
Nembo ya mazungumzo ya muungano unaoitwa wa Jamaica kati ya CDU/CSU(nyeusi), FDP (Manjano) na walinzi wa mazingira die Grüne wanaojitambulisha na rangi ya kijaniPicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

 Mazungumzo huenda yakadumu wiki kama si miezi

Mada hizo ni pamoja na suala la wakimbizi na kinga ya ukimbizi, sawa na nishati na sera kuelekea mabadiliko ya tabia nchi. Hii leo wawakilishi wa chama cha kiliberali cha FDP wanakutana na walinzi wa mazingira die Grüne. Na ijumaa ndipo duru ya kwanza itakayowakutanisha wawakilishi wa pande zote nne itakapoitishwa mjini Berlin. Kwakua misimamo ya pande hizo nne inatofautiana mno, wadadisi wanakadiria mazungumzo hayo yatadumu muda mrefu  kupita kiasi. Binafsi kansela Angela Merkel anakadiria wiki kadhaa zitahitajika. Kuna wanaokadiria mazungumzo yanaweza kuendelea hadi mwakani.

NMwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/dpa/Reuters

Mhariri:Josephat Charo