1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vijembe vyachangamsha bunge Uingereza

13 Julai 2016

David Cameron ahudhuria kikao cha bunge la Uingereza kwa mara ya mwisho akiwa kama Waziri Mkuu na kukigeuza kikao hicho cha masuali na majibu kuwa mseto wa kupongezana, kutolewa kwa shukrani,vijembe, shutuma na shangwe

https://p.dw.com/p/1JONd
Picha: TV Out/via Reuters

David Cameron leo amehudhuria kikao cha bunge la Uingereza kwa mara ya mwisho akiwa kama Waziri Mkuu wa nchi hiyo na kukigeuza kikao hicho cha masuali na majibu kuwa mseto wa kupongezana, kutolewa kwa shukrani,vijembe, shutuma na shangwe.

Kikao hicho kilimalizika kwa kushangiliwa kwa Cameron mwenye umri wa miaka 49 ambaye anaachia madaraka baada ya wapiga kura kuukataa ushauri wake na kuamuwa kujitowa Umoja wa Ulaya. Hivi sasa anawasilisha rasmi baruwa yake ya kujiuzulu kwa Malkia Elizabeth wa Pili na baadae kukabidhi madaraka kwa Theresa May.

Amesema atakosa shangilio la wananchi na atavikosa pia vijembe vya wapinzani na kuahidi kuangalia mijadala ya siku za usoni akiwa kama mbunge wa kawaida wa chama cha Consevative.

Pia alijidhihaki kwa kuwakumbusha wabunge juu ya kijembe alichomtupia waziri mkuu wa zamani Tony Blair wa chama cha Labour wakati kiongozi huyo alipokuwa akiondoka madarakani:

(O-Ton Cameron)

"Jambo la mwisho ambalo ningelipenda kulisema ni kwamba unaweza kufanikisha vitu vingi katika siasa kwamba unaweza kufanya mambo mengi.Na yote hatimae inakuwa ni kuhusu huduma kwa wananchi na kuhusu maslahi ya taifa.Kwa kweli hakuna kitu kisichowezekana iwapo unakiwekea nia na kwa vyo vyote vile kama vile nilivyowahi kusema ,niliwahi kuwa mtu niliyewekewa matumaini."

Wasia kwa May

Mojawapo ya vijembe viivyochangamsha kikao hicho ilikuwa ni kati ya Cameron na kiongozi wa chama cha Labour Jeremy Corbyn ambapo ameudhihaki mzozo wa uongozi unaoendelea katika chama cha Labour kwa kumwambia Corbyn kwamba wahafidhina walikuwa na kujiuzulu,kuteuliwa,ushindani na kutawazwa wakati chama cha Labour bado kinapambana na kanuni za ongozi wa chama hicho.

Theresa May anayechukuwa nafasi ya Wazir Mkuu David Cameron.
Theresa May anayechukuwa nafasi ya Wazir Mkuu David Cameron.Picha: Getty Images/C. Furlong

Cameron amemuhimiza mrithi wake Teresa May kuiweka Uingereza karibu na Umoja wa Ulaya kadri inavyowezekana.

Kiongozi mpya wa Uingreza Theresa May ambaye alikuwa waziri wa mambo ya ndani kwa miaka sita atakuwa na kibaruwa kigumu cha kuituliza nchi hiyo na masoko ya fedha kufuatia vurugu kubwa zilizosababishwa na uamuzi wa kura ya maoni nchini Uingereza Juni 23 kujitowa Umoja wa Ulaya.

Baada ya Cameron kujiuzulu rasmi May mwenye umri wa miaka 59 atakwenda kwenye kasri la Malkia ambapo Malkia atamtaka aunde serikali.

Mwandishi: Mohamed Dahman /AP/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef