Vijana wajitokeza kushiriki mdahalo wa Maoni Mtaani
19 Oktoba 2022Kumekuwa na maoni yaliyochepuka katika mikondo mbalimbali hasa katika eneo lilomulika kwa nini vijana wengi wanaonekana kuachwa nyuma katika dhima ya uongozi katika wakati ambapo kunashuhudia mabadiliko makubwa katika sekta ya teknolojia na mawasilinao.
Masuala yaliyogusiwa kukua kwa mitandao ya kijamii pamoja na maendeleo ya kasi ya sekta ya habari na mawasiliano ni miongoni mwa mambo mengine pia yaliyowashughulisha wazungumzaji kwenye mdahalo huo ambao pia umewashirikisha watu wa kada mbalimbali.
Katika salamu zake, za awali mkuregenzi wa vipindi wa DW, Nadjia Shuk aligusia jukumu muhimu la idhaa ya DW Kiswahili kupasha habari zisizo na upendeleo huku zikiwagusa makundi yote ya jamii ikiwamo vijana.
Akiwa na ujumbe wa vijana na taifa la leo, mkurugenzi mtendaji wa ITV na Radio One, Joyce Muhavile aliwakumbusha vijana hao namna wanavyopaswa kufumbua macho yao na kuchangamkia kile wanachoona mbele yao.
Mmoja wa wazungumzaji kwenye mdahalo huo, Lovelet Lwakatare ambaye ni mshauri wa siasa na mawasiliano ya umma aliwatupia lawama baadhi ya watunga sera na wanasiasa kwa kuendelea kuwatumia vijana kama daraja la kufanikisha ajenda zao.
Baadhi ya vijana hao wameonyesha kiu ya kutaka kuchomoza kwenye masuala ya uongozi na hatma ya taifa lao, na wanaamini kwamba kupitia kwenye midahalo kama hii, uwezekano wa kuzifikia ndoto zao ni mkubwa mno.
Katika michango yao vijana wanataka kufunguliwe milango itayowezesha kuwa na usemi katika kuamua hatma ya maisha yao.