Vijana wajadili kuhusu utengamano wa wageni
17 Aprili 2012Vijana 100 kutoka pande zote za Ujerumani wamehudhuria kongamano hilo. Wametembezwa katika ofisi ya Kansela na katika chumba cha habari cha bunge la Ujerumani. Nusu ya vijana hao wana nasaba ya kigeni huku wengine wakiwa Wajerumani wazawa, kama anavyoeleza Maria Böhmer ambaye ni mkuu wa masuala ya uhamiaji na utengamano katika serikali ya Kansela Angela Merkel. Vijana wanaohudhuria kongamano la siku mbili mjini Berlin wamekuja kujadili kuhusu namna ya kuwaingiza katika jamii vijana kutoka nje.
Johannes Zieseniß, ambaye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ni mmoja wa vijana hao. Matumaini yake yalikuwa kupata nafasi ya kuzungumza na vijana wenzake na anatamani serikali itachukulia kwa makini masuala yaliyojadiliwa.
Ujasiri, uwazi na uvumivilvu vyahitajika
Kansela Angela Merkel, ambaye pia alikuwepo katika kongamano hilo, aliwahakikishia vijana waliohudhuria kwamba anapenda kusikia maoni yao ya wazi na si maneno ya kupamba tu. "Kwa sababu hiyo ninawaomba muwe wazi kabisa katika majadiliano hayo na msiwe na wasiwasi kusema jambo ambalo huenda halikubaliki na wote," alieleza Merkel. "Mambo yanayohitajika kuwezesha utangamano ni uwazi, uvumilivu na kwa sehemu fulani ujasiri."
Merkel aliendelea kusema kwamba ni lazima kuzungumza pia juu ya dhana potofu walizonazo watu kuhusu watu kutoka jamii nyingine. Akitoa mfano, Merkel alisema kwamba, mhitimu mmoja wa shule ya sekondari alimweleza kuwa hakuwahi kuitwa kwa ajili ya kufanyiwa mahojiano ya kutafuta kazi kwa sababu tu jina lake ni la Kituruki. Merkel aliwahimiza vijana kuzungumza juu ya tatizo hilo akikumbusha kwamba ni kwa njia hiyo tu mambo yataweza kubadilika.
Vijana watakiwa kujenga utamaduni wa kuwakaribisha wageni
Ümmühan Ciftci ni mwanafunzi wa chuo kikuu mwenye uraia wa Uturuki licha ya kwamba amezaliwa Ujerumani. Miaka miwili iliyopita mwanafunzi huyo alianzisha shirika linalowapa watu kutoka nje mafunzo kuhusu mfumo wa elimu unaofuatwa hapa Ujerumani. Wazazi wa Ümmühan waliamua kumpeleka katika shule ya sekondari, licha ya kwamba palikuwa na watu waliowakatisha tamaa. Lakini kwa sababu walifuata uamuzi wao, leo hii binti yao ni mwanafunzi wa chuo kikuu. Ümmühan alilihudhuria kongamano akiwa na matarajio makubwa ya mkupata hamasa zaidi kwa ajili ya kazi anayoifanya ya kuelimisha watu. "Ni lazima sisi vijana tutiwe moyo. Tunataka tumalize kongamano hili tukisema kwamba mazungumzo yametusaidia na hivyo tutaendelea na juhudi zetu."
Washiriki wa kongamano hilo waliweza kuchagua kuhudhiria warsha zilizotolewa katika nyanja za elimu, vyombo vya habari, migogoro ya vizazi na kujitolea kwa watu katika jamii. Maria Böhmer, mkuu wa masuala ya uhamiaji na utengamano wa hapa Ujerumani, alieleza kwamba lengo kuu la warsha hizo lilikuwa kuwafanya vijana waondokane na hali ya kuwa na wasiwasi juu ya watu wengine na badala yake kujenga utamaduni wa kuwa wazi na kuwakaribisha watu kutoka nje.
Mwandishi: Nina Werkhäuser
Tafsiri: Elizabeth Shoo
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman