1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vijana nchini Ghana wataka mageuzi ya kijamii na kiuchumi

Zainab Aziz Mhariri: Daniel Gakuba
4 Agosti 2021

Vijana nchini Ghana wanataka maswala ya nchi hiyo yarekebishwe na hivyo basi wameanzisha kampeni mtandaoni kwa jina #FixTheCountry inayolenga kuishinikiza serikali.

https://p.dw.com/p/3yXjF
Screenshot Twitter Fixthecountry
Picha: Twitter@Ghfixthecountry

Harakati hizo za hashtag #FixTheCountry na nyingine kadhaa tofauti zilianzishwa mnamo mwezi Mei mwaka huu, kwenye mitandao ya kijamii na vijana wa Ghana wakitaka mageuzi ya kijamii na kiuchumi. Kampeni hiyo ilienea na kupata umaarufu kwa haraka, maelfu walijiunga na harakati hiyo ambayo inalenga serikali ya Ghana inayoonekana kuwa haiwajibiki vizuri.

Parlament in Accra, Ghana
Bunge la GhanaPicha: DW/I. Kaledzi

Je! Vipi harakati hizo zimetoka mitandaoni na kuingia mitaani?. Watu walio nyuma ya hashtag hiyo ambao wanasema wao sio wanasiasa walitoa mwito wa kufanyika maandamano mitaani mnamo Mei 9. Lakini walishindwa kuendesha maandamano hayo baada ya polisi kupata amri ya mahakama iliyowazuia kufanya maandamano kwa sababu za kiusalama wakati huu wa janga la COVID -19.

Mnamo Julai 6, mabango yenye hashtag hiyo ya #FixTheCountry yalionekana yamebebwa kwenye maandamano ya kupinga serikali huko mjini Accra yaliyokuwa yameitishwa na chama cha upinzani cha National Democratic Congress (NDC) na wafuasi wa harakati za hashtag #FixTheCountry walijiunga kudai haki kwa watu wawili waliopigwa risasi na polisi katika mkoa wa Ashanti kusini mwa Ghana. Waandamanaji pia walikuwa wakipinga kupigwa vibaya mwanaharakati wa vijana Ibrahim "Kaaka" Mohammed mnamo Juni 29.

Wafuasi wa chama cha upinzani cha NDC - National Democratic Party
Wafuasi wa chama cha upinzani cha NDC - National Democratic PartyPicha: Cristina Aledhuela/AFP

Wanaharakati hao wamepanga kufanya maandamano yao, leo Jumatano 04.08.2021. Ernesto Yeboah mwanaharakati wa kundi la Economic Fighters League ameiambia DW kwamba vuguvugu la sasa linatokana na hisia jumla kati ya vijana kutosikilizwa na wanaosimamia nchi. Amesema vijana wana njaa, mambo ni mabaya, mambo ni magumu na kwa jumla maisha ni magumu na wala hali hiyo haigongi vichwa vya habari. 

Mara zote Ghana husifiwa kama nchi yenye demokrasia thabiti katika eneo tete la Afrika Magharibi. Uchaguzi wa Rais mnamo Desemba mwaka jana ulizingatiwa kuwa ni huru na ulifanyika kwa haki kwa mujibu wa waangalizi wote waliosimamia uchaguzi huo. Lakini kura hiyo ilizua mivutano ya kisiasa. Rais Nana Akufo-Addo alishinda muhula wa pili, lakini chama chake kiliwashinda wapinzani kwa idadi ndogo tu ya wabunge.

Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo
Rais wa Ghana Nana Akufo-AddoPicha: AP Photo/picture alliance

Vijana nchini Ghana wanazidi kukabiliwa na ukosefu wa fursa. Nchi hiyo imezongwa na mzigo wa kuongezeka kwa deni la serikali na mapato yamepungua kutokana na athari za janga la corona, hivyo basi serikali imeweka kodi mpya iliyosababisha kuongezeka kwa bei ya mafuta ambayoimesababisha kupanda kwa gharama za bidhaa na huduma muhimu.

Kulingana na utafiti wa taasisi ya Brookings, wakati uchumi wa Ghana ulinawiri kwa kasi katika miongo miwili iliyopita, upatikanaji wa ajira haukufana. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Ghana ina watu milioni 31 na zaidi ya nusu ya idadi ya watu hao ni vijana walio chini ya miaka 25, wazazi wengi hawana uwezo wa kuwapeleka vijana wao kujiunga na vyuo vikuu na theluthi moja ya vijana hawana kazi au hata mafunzo ya kitaalam. Na juu ya yote janga la maambukizi ya virusi vya corona limeongeza maumivu na hasira miongoni mwa vijana wa nchini Ghana.

Chanzo:/ https://p.dw.com/p/3yUAl