Vijana Afrika walaghaiwa kucheza soka Ulaya
8 Novemba 2013Jean-Claude Mbvoumin, mchezaji wa zamani wa Cameroon ambaye ni kiongozi wa shirika la Culture Foot Solidaire (CFS), amesema kuwa takribani wachezaji 15,000 vijana walipelekwa ng'ambo kila mwaka kupitia njia bandia. Anasema mawakala, ambao kila mara wao hutumia vitambulisho bandia vinavyodaiwa kutolewa na vilabu vya UIaya, huzungumza na wazazi wa wachezaji wa soka, huku wakiwaahidi mkataba mzuri ng'ambo kwa kupewa ada ya karibu euro 3,000 na 10,000.
Na inakuwa rahisi kwa sababu barani Afrika, kila mchezaji huwa na ndoto ya kuwa Samuel Eto'o, Didier Drogba, Yaya Toure na wengine wengi. Wazazi kisha hulipa pesa hizo bila kuwa na ufahamu wa kutosha. Wanafikiri watoto wao watafanikiwa haraka katika kandanda, na kuwaacha watoto hao mikononi mwa watu wasiojulikana.
Shirikisho la soka ulimwenguni FIFA lilianzisha sheria kali kuhusu uhamisho wa kimataifa wa wachezaji, hasa ule unaowahusisha wachezaji wa chini ya miaka 18 ambao wanapewa idhini tu, mara baada ya orodha ndefu ya masharti inapokamilishwa.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo