Vifo zaidi Elgeyo Marakwet - Baringo, Kenya
28 Februari 2022Hali bado ni tete katika maeneo ya mpakani mwa Elgeyo Marakwet na Baringo ambapo watu wanane, wawili kati yao wakiwa Watoto waliuwawa kufuatia mapigano kati ya jamii mbili za eneo hilo. Afisa wa polisi aliyekuwa akishika doria ni kati ya majeruhi walioripotiwa.
Kamishna wa kanda ya bode la ufa Maalim Mohammed amekanusha madai kwamba zaidi ya mifugo elfu moja waliibiwa kwenye ghasia hizo. Ametaja baadhi ya vigezo vinavyotatiza oparesheni za kiusalama eneo hilo kuwa mila na tamaduni za jamii hizo.
Watetezi wa haki za binaadam eneo hilo wanaendelea kulalamikia kuwa mashambulizi ya mara kwa mara yametatiza uthabiti wa kijamii, shughuli za kawaida za kiuchumi, na yameathiri hali ya masomo ikizingatiwa kuwa baadhi ya wanafunzi wanatarajiwa kuanza mitihani yao ya kitaifa katika muda wa wiki moja ijayo.
Kamishna wa kanda Maalim Mohammed amesisitiza kuwa oparesheni ya kuwapokonya raia silaha bado inaendelea eneo hilo. Amesema matumizi ya polisi wa akiba wanaoelewa na kufahamu hali na maeneo hayo vyema zaidi, ni mikakati waliyoiweka, na tayari wameshayasajili majina ya watu themanini kwa wizara ya usalama wa ndani.
Siku ya jumatano viongozi hawa wanatarajiwa kukutana kutathmini hali maeneo hayo yaliyoathirika na ukosefu wa usalama.
Mwandishi: Wakio Mbogho, DW, Nakuru.