1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vifo vyaitikisa Iraq tena

Tuma Provian Dandi5 Oktoba 2007

Iraq imeendelea kukumbwa na mauaji ya kivita dhidi ya raia na baadhi ya watu wanaosemekana kuwa wanaharakati wapiganaji, baada ya ndege za jeshi la Marekani kufanya shambulio kubwa

https://p.dw.com/p/C7ia
Rais George W. Bush wa Marekani
Rais George W. Bush wa MarekaniPicha: AP

Ikihakiki vifo hivyo, Wizara ya Ulinzi ya Iraq imesema watu 17 wameuawa, 27 kujeruhiwa na wengine wanane wahawajulikani waliko baada ya shambulizi lililofanywa ndege za kijeshi za Marekani nchini humo.

Taarifa zaidi imeeleza kwamba shambulio hilo lililotokea kwenye Jiji la Baquba, limehusisha vifo vya wanawake na watoto pamoja na watu wengine katika kijiji cha Al Jaysani karibu na mji wa Al Khalis unaokaliwa na watu wa Kabila la Kishia, usiku wa kuamkia leo.

Shambuli hilo la ndege za kijeshi za Marekani pia limehusisha uharibifu wa nyumba nne.

Raia mmoja anayeitwa Ahmed Mohammed, amesema majeruhi 15 wameweza kupata msaada na kufikishwa katika hospitali moja iliyoko mjini Baghdad, na kwamba wengine wamebaki kwenye eneo la tukio na mipango ilikuwa ikiendelea ili kuwapatia matibabu.

Wakitoa maelezo kuhusu shambulio hilo, maofisa wa kijeshi wa Marekani wamekiri kufanya mauaji kwa watu 25 waliohisiwa kwamba ni raia wenye asili ya Iran, ambao wamekuwa wakitoa misaada mbalimbali ikiwemo silaha kwa vikundi vya wanamgambo nchini Iraq.

Taarifa imeendelea kueleza kwamba kabla ya shambulizi la vikosi vya Marekani, watu hao waliosemekana kuwa wanamapinduzi wa Iran, walirusha roketi ambalo hata hivyo halikuelezewa kuhusu madhara yake dhidi ya vikosi vya Marekani au raia wa Iraq.

Majeshi ya Marekani yanasema kwamba kwa kipindi kirefu vikosi vya wanaharakati wa Iran vinavyoitwa Vikundi Maalumu, vimekuwa na ushirikiano wa karibu na wanamgambo wa Iraq ambapo kwa pamoja wanashiriki katika vitendo vya kigaidi yakiwemo mashambulizi dhidi ya majeshi ya marekani na yale iraq, pamoja na kujitoa muhanga.

Vikundi hivyo vinavyosemekana kutoka Iran huwa na lengo la kuwasaidia wanamgambo wa Iraq wanaounga mkono ngome ya mpiganaji mkuu Moqtada Al Sadr.

Majeshi ya Marekani yamesisitiza kwamba kamwe hayataacha kufanya mashambulizi dhidi ya wapiganaji hao, na kwamba yapo hapo kwa ajili ya kuisaidia serikali ya Iraq hadi hali itakapokuwa ya kuridhisha.

Pia majeshi hayo yamedai kukamata mabomu ya kisasa yanayorushwa kwa kutumia ndege za kivita au roketi, yaliyotengenezwa Iran kwa ajili ya kufanya uharibifu wa binadamu nchini Iraq.

Mashambulizi hayo yamekuja wakati ambapo Iran na Marekani zinavutana kuhusu raia mmoja wa Iran Bwana Mahmoudi Farhadi anayeshikiliwa na majeshi ya Marekani kwa siku 14 kutokana na tuhuma za jasusi.

Makamanda wa Marekani wanasema kwamba Bwana Farhad ni mmoja wa watu wanaowasaidia wanamgambo wa Iraq kupitia vikosi maalumu vya wapiganaji.