1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vifo vya watoto kutokana njaa vyaongezeka Pembe ya Afrika

5 Oktoba 2011

Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia watoto, UNICEF, limeonya juu ya ongezeko la vifo vya watoto katika eneo la Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika kutokana na utapiamlo.

https://p.dw.com/p/12loy
Wasomali wakisubiri kupewa chakula MogadishuPicha: picture-alliance/dpa

Katika mahojiano aliyokuwa nayo na shirika la habari la Ujerumani, DPA, Lake amesema kulingana na hali ilivyo katika eneo hilo, watoto zaidi wanaweza kufa kama hawatapelekewa misaada. Mkuu huyo wa UNICEF amezungumzia janga baya kabisa la kibinadamu kuwahi kushuhudiwa ulimwenguni.

Kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifa watu milioni 13 wameathirika na baa la njaa Afrika Mashariki, wakiwemo watoto milioni kadhaa. Nchini Somalia pekee watoto takriban 450,000 wanakabiliwa na utapiamlo mkali, 200,000 kati yao wakikabiliwa na kitisho cha kifo, kutokana na hali mbaya mno inayowakabili. Tayari maelfu kadhaa ya watu walikufa miezi kadhaa iliyopita na inakisiwa kila mtu wa pili aliyekufa alikuwa mtoto. Inahofiwa hali itazidi kuwa mbaya kadri siku zinavyopita.

Somalia Hungersnot Schlange von Menschen vor Ausgabe von Lebensmitteln in Mogadishu
Wanawake na watoto wakisubiri chakula kusini mwa SomaliaPicha: dapd

Msemaji wa shirika la UNICEF, Marixie Mercado, amethibitisha kwamba kitisho kwa maisha ya watoto katika eneo la pembe ya Afrika kinaongezeka, hasa nchini Somalia.

"Watu takriban milioni 13 wanahitaji msaada Somalia, Kenya na Djibouti ambako msaada unahitajika kwa dharura kwa ajili ya watoto 300,000 walio chini ya umri wa miaka 5 wanaokabiliwa na utapiamlo. Hii inajumuisha watoto 160,000 kusini mwa Somalia wanaoweza kufa katika wiki zijazo kama hawatapata msaada wa dharura."

Shinikizo ni kubwa

Mkurugenzi wa shirika la UNICEF, Antony Lake, amesema wanakabiliwa na shinikizo kubwa la kuwasaidia watoto na mahitaji ya chakula, hususan wakati huu ambapo magonjwa ya kuambukiza kama vile surua na kipindupindu yanaenea. Surua huua sana watoto wakati wa majanga kama haya.

Lake aliyewahi kuwa mshauri wa masuala ya usalama wa rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, amekuwa akiliongoza shirika la UNICEF tangu mwezi Mei mwaka uliopita. Ametoa mwito misaada itolewe.

"Wasiwasi wetu ni kwamba hamasa iliyokuwepo kuhusu hali ya njaa katika pembe ya Afrika kwa wakati huu imepotea. Lakini watu wengi wanaendelea kuteseka sana katika eneo hilo kiasi kwamba hatupaswi kusahau hivi hivi," amesema mkurugenzi huo.

Juhudi za uokozi

Watoto wanaweza kuokolewa kama watapa matibabu kwa wakati ufaao. Shirika la UNICEF linadhamini vituo 800 vya kutoa chakula nchini Somalia, ambako watoto takriban 35,000 wenye utapiamlo wanapata matibabu na kuangaliwa. Shirika hilo pia limeweka mkahawa wa kuhahama, ambapo chakula kama vile mchanganyiko wa maharagwe na mahindi, mafuta na matunda hugawanyiwa watoto.

Somalia Hungersnot
Wasomali wakipewa chakulaPicha: dapd

Msemaji wa shirika la UNICEF, Marixie Mercado, amesema wananafanya kazi kuwafikia zaidi ya watoto milioni 10 katika eneo la Pembe ya Afrika na Afrika Mashariki kuwadunga chanjo wanazohitaji, kuwapelekea maji zaidi ya watu milioni 4 na kuwapelekea vifaa vya kupambana na utapiamlo.

"Lakini hayo yote yanahitaji msaada uendelee kutolewa na wafadhili na tusizuiliwe kuwafikia watu wanaohitaji msaada wetu. Tunahitaji kuangalia mikakati ya muda mrefu na tuweke mipango ili watu waweze kukabiliana na athari za ukame na mafuriko bila kuwa maskini."

Ukame katika eneo la Afrika Mashariki unaelezwa kuwa mbaya kabisa kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 60 iliyopita.

Mwandishi: Josephat Charo/DPA

Mhariri: Hamidou Oummilkheir