Vifo kutokana na Ebola vyapindukia 1000 DRC
25 Machi 2019Matangazo
Wizara ya afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesema idadi ya waliokufa kutokana na maradhi ya Ebola imepindukia 1000, wakati mripuko wa ugonjwa huo ukiendelea kuiandama nchi hiyo.
Waziri wa afya Oly Ilunga Kalenga amesema pamoja na idadi hiyo ya vifo, mamia ya familia za Wacongo zinaendelea kuteswa na maradhi hayo hatari, huku pia idadi ya mayatima ikiongezeka.
Mripuko wa hivi karibuni katika eneo la Mashariki mwa Congo umeuwa watu 629, lakini watu wengine 320 wameweza kunusurika. Hali kadhalika, watu 91,000 wamepatiwa chanjo dhidi ya Ebola tangu mwezi Agosti mwaka jana.
Maafisa wa Congo wamesema wafanyakazi wa mashirika ya afya wametaabika katika shughuli zao Mashariki mwa Nchi, ambako kumetapakaa makundi yenye silaha.