VIENNA : Mzozo wa nuklea wa Iran bado moto
20 Februari 2007Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya nuklea amesema Iran inaweza kuwa katika nafasi ya kurutubisha uranium katika kiwango cha viwandani katika kipindi kisichozidi miezi sita hadi 12 ijayo.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomu Mohammed El Baradei amesema kwamba Iran yumkini ikawa na kipindi cha takriban miaka mitano kabla ya kuwa na uwezo wa kutengeneza bomu la nuklea.El Baradei alitamka hayo katika mahojiano na gazeti la Financial Times ambapo pia amesema Iran yumkini ikashindwa kutimiza agizo la Umoja wa Mataifa kwa muda wa mwisho wanaotakiwa kusitisha urutubishaji wa uranium hapo kesho.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeiwekea vikwazo Iran miezi mwili iliopita kujaribu kuilazimisha kusitisha shughuli zake za urutubishaji.
El Baradei anatazamiwa kukutana na msuluhishi wa masuala ya nuklea wa Iran Ali Larijani mjini Vienna leo hii.