VIENNA: Mzozo wa Iran bado haujapata ufumbuzi
11 Agosti 2005Shirika la nishati ya nyuklia la umoja wa mataifa, linajadili pendekezo la umoja wa Ulaya, linalolenga kuishawishi Iran kusitisha shughuli zake zote za nyuklia. Azimio hilo linalozungumziwa na magavana wa bodi ya shirika hilo mjini Vienna, linaelezea wasiwasi mkubwa kufuatia hatua ya Iran kuanza tena kurutubisha madini ya uranium.
Lakini azimio hilo lililodhaminiwa na umoja wa Ulaya linataka swala la Iran liwasilishwe mbele ya baraza la usalama la umoja wa mataifa, kwa uwezekano wa kuwekewa vikwazo.
Afrika Kusini imependekeza uchafu unaotoka kwenye kiwanda cha Isfahan usafirishwe katika mataifa ya kigeni kabla kuanza kutumiwa kurutubishia uranium, kiungo muhimu cha kutengenezea silaha za nyuklia. Lakini wanadiplomasia wanaufuatilia mkutano huo mjini Vienna wamesema pendekezo hilo linalonuia kuutanzua mzozo huo wa Iran, huenda lisikubaliwe.
Mazungumzo hayo yanafanyika siku moja baada ya Iran kuondoa mihuri ya umoja wa mataifa katika kinu chake cha nyuklia cha Isfahan, hivyo kukiruhusu kuanza kazi kamili. Kufunguliwa tena kwa kinu hicho ni hatua ya mwanzo itakayoiwezesha Iran kusafisha madini ya uranium ambayo yanaweza kutumiwa kutengeneza silaha za nyuklia.