VIENNA: Larijani aonya juu ya matumizi ya nguvu kuumaliza mzozo wa nyuklia wa Iran
21 Februari 2007Mpatanishi mkuu wa Iran katika mzozo wa nyuklia, Ali Larijani, ameonya kwamba mzozo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran hauwezi kutanzuliwa kutumia vitisho vya matumizi ya nguvu.
Larijani aliyasema hayo jana mjini Vienna Austria baada ya kukutana na kiongozi wa shirika la kimataifa la kuzuia utapakazaji wa silaha za kinyuklia, IAEA, Mohamed El Baradei.
Larijani alitoa matamshi hayo siku moja kabla kumalizika muda uliowekwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwa Iran ikomeshe urutubishaji wa madini yake ya uranium. Alisema jaribio lolote la kuilazimisha Iran litakabiliwa kwa hatua zinazofaa.
El Baradei anatarajiwa kuripoti kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kesho kutwa Ijumaa ikiwa Iran imesitisha urutubishaji wa uranium.
Matokeo ya uchunguzi wake yatajadiliwa na kikao cha bodi ya magavana wa shirika la IAEA mwezi ujao.
Rais wa Iran, Mahmud Ahmadinejad alisema nchi yake iko tayari kusitisha urutubishaji wa uranium ikiwa mataifa ya magharibi nayo yatafanya hivyo.