Verstappen aweka historia katika Formula One
16 Mei 2016Verstappen alitumia fursa ya ajali ya iliyotokea katika mzunguko wa kwanza iliyoyalazimu magari yote mawili ya timu ya Mercedes kujiondoa mashindanoni.
Katika mshindano yake ya kwanza ndani ya gari la timu ya Red Bull baada ya kupandishwa ngazi kutoka timu ya Toro Rosso, Mholanzi huyo mwenye umri wa miaka 18 alionyesha utulivu chini ya shinikizo wakati aliyastahili mashambulizi yote na kupata ushindi wa ajabu katika mashindano yake ya 24 ya F1. Madereva wa timu ya Ferrari Kimi Raikonen na Sebastian Vettel walipanda jukwaani katika nafasi ya pili na tatu.
Lakini ushindi huo ulighubikwa na uhasama uliodhihirika kati ya madereva wawili wa Mercedes Lewis Hamilton na Nico Rosberg ambao waligongana katika mzunguko wa kwanza na kuyaaga mashindano.
Madereva wote wawili walionekana kunyoosheana kidole cha lawama lakini wakubwa wa Mercedes wamesalia kimya kuhusu suala hilo wakisema madereva hao hawatachukuliwa hatua na badala yake watashauriana kuhusu namna ya kuendelea mbele katika mashindano yajayo.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Yusuf Saumu