1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Venezuela yazidi kufukuta

21 Julai 2017

Watu wawili wameuawa katika mgomo na maandamano yanayofanyika nchini Venezuela ya kupinga mpango wa Rais Nicolas Maduro wa kuiandika upya katiba. Wakati huohuo mwakilishi wake katika UN pia emejiuzulu akiunga mkono raia.

https://p.dw.com/p/2gwEe
Venezuela - Streik - Krise
Picha: Reuters/C. G. Rawlins

Mwanadiplomasia na mwanasheria wa kimataifa nchini humo, Isaias Medina, amejiuzulu kutokana na mateso dhidi ya raia na kile alichokiita kuwa ni ugaidi unaofanywa na serikali na ukiukwaji wa katiba unaofanywa na serikali ya Maduro, na kumtaka rais huyo kuondoka madarakani. 

Mgomo na maandamano yaliyodumu kwa masaa 24 hapo jana, yaliathiri baadhi ya maeneo katika mji mkuu wa Venezuela na maeneo mengine, ambayo ni pamoja na mji wa pili kwa ukubwa wa Maracaibo, huku maduka na biashara zikiharibiwa na usafiri wa umma ukizorota.

Polisi na wanajeshi walifyatua mabomu ya machozi na risasi za bandia dhidi ya waandamanaji waliofunga baadhi ya mitaa ya Caracas usiku mzima kwa marundo ya takataka pamoja na kuchoma moto vibanda vya polisi. 

Mwendesha mashtaka amesema, kijana wa miaka 24 aliuawa katika viunga vya mji wa Caracas na mwingine wa miaka 23 akiuawa katika mji wa Valencia. Hata hivyo hakuweka wazi nani aliyefanya mauaji hayo. Vifo hivi vinafikisha idadi ya waliokufa katika maandamano ya kuipinga serikali tangu mwezi Aprili kufikia 99.

Venezuela Proteste
Waandamanaji wanamtaka Rais Maduro kuondoka madarakani na si mazungumzoPicha: picture-alliance/dpa

Baadhi ya waandamanaji waliofunga mitaa katika mji wa Caracas wameeleza kuchoshwa na serikali, kutokana na upungufu wa chakula, kukosekana dawa na vijana kutojua mustakabali wa maisha yao.

Waandamanaji hao pia waliweka vizingiti vya mawe kuwazuia wafanyakazi wa kituo cha televisheni cha serikali cha VTV, ambao waliokolewa kwa msaada wa polisi.

Takribani waandamanaji 370 walikamatwa mjini Caracas na majimbo mengine manne, hii ikiwa ni kulingana na ripoti ya taasisi isiyo ya kiserikali ya Foro Penal.

Mwanadiplomasia na mwakilishi wa Venezuela kwenye Umoja wa Mataifa ajiuzulu.

Wakati hayo yakiendelea, mwanadiplomasia wa nchi hiyo, ambaye pia aliwahi kuwa balozi katika ujumbe wa Venezuela kwenye Umoja wa Mataifa, Isaias Medina, amesema amechukua hatua ya kujiuzulu ili kuunga mkono hatua ya raia ya kumpinga Maduro. Medina ambaye pia ni mwanasheria wa kimataifa ameliambia shirika la habari la Associated Press jana usiku kwamba siku 100 za mwisho, ambazo watu 15,000 walijeruhiwa na zaidi ya 100 kuuawa zimemsababishia athari kubwa.

Amesema itakuwa ni unafiki kusalia hapo wakati anashindwa kuwakilisha maadili ya mikataba ya Umoja wa Mataifa, huku akimtaka Rais Maduro kuondoka madarakani, ili kuruhusu serikali mpya kuchukua nafasi na kuanza kufanya majukumu yake.

Medina amesema si sawa kabisa kwa Venezuela kuwa mwanachama wa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa wakati yenyewe ni mkiukaji wa haki hizo, pamoja na kuwa mwenyekiti wa chombo hicho, wakati yenyewe ikishindwa hata kuruhusu watu wake kufanya maamuzi.

Maduro anakabiliwa na ghadhabu kutoka kwa raia kutokana na mkakati wake wa kuchagua chombo kipya kitakachojulikana kama bunge la katiba itkayoandika upya katiba. wakosiaji wanasema hatua hiyo ni kama ukwapuaji wa mamlaka. Rais Donald Trump wa Marekani ameonya kuhusu hatua za kiuchumi zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya venezuela, iwapo kura hiyo itapigwa.

Hata hivyo Maduro amesema tishio hilo la Trump, limemuongezea nguvu zaidi ya kuandaa kura hiyo kuliko wakati mwingine wowote.

Mwandishi: Lilian Mtono/AP/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef