Venezuela yamfukuza balozi wa Ujerumani
7 Machi 2019Wizara ya mambo ya nje imempa balozi huyo wa Ujerumani Daniel Kriener masaa ya 48 ya kuondoka nchini humo kwa madai ya kuingilia masuala ya ndani ya Venezuela. Balozi Kriener alionekana uwanja wa ndege wa Caracas akimkaribisha Juan Guaido wakati alipokuwa akirejea nchini humo siku ya Jumatatu.
Guaido amesema, hatua ya kufukuzwa kwa Kriemer itachukuliwa kama kitisho dhidi ya ulimwengu huria. Kriener alikuwa miongoni mwa mabalozi wengine waliomkaribisha Guaido, anayetambuliwa na mataifa zaidi ya 50 kama rais wa mpito, lakini ni yeye pekee aliyefukuzwa na ni mtu asiyetakiwa tena nchini humo.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema hatua hiyo inayotajwa na wachambuzi wa Venezuela kama ujumbe kwa walio mstari wa mbele kuipinga serikali ya Maduro inazidi kudhoofisha hali ya mambo.
Huku hayo yakiendelea, Makamu wa rais wa Marekani Mike Pence ametangaza serikali yake kuongeza vikwazo vinavyolenga kumshinikiza Maduro kuondoka mamlakani kwa kufuta vibali 77 vya kusafiria kwa watu wenye mahusiano na Maduro. Alinukuliwa akisema "Ninawaahidi Wamarekani wenzangu tutaendelea kuwa imara. Na hii leo wizara ya mambo ya nje inatangaza kuwafutia vibali vya kusafiria raia 77, wakiwemo maafisa wa serikali ya Maduro na familia zao. Tutaendelea kuiwajibisha serikali ya Maduro hadi pale taifa hilo litakapokombolewa".
Idadi ya raia wa Venezuela waliokumbwa na kadhia hiyo ni zaidi ya 250 sasa. Katika hatua nyingine, mwandishi wa habari, Cody Weddle raia wa Marekani, aliyetiwa kizuizini na vikosi vya usalama vya Venezuela kwa takriban masaa 12 naye anatarajiwa kurejeshwa kwao. Tukio hilo pia limelaaniwa vikali na makundi ya utetezi na kulitaja kama shambulizi dhidi ya uhuru wa kujieleza.
Mshauri wa masuala ya usalama John Bolton naye amezionya taasisi za kifedha za kigeni zitakazojihusisha na shughuli za haramu za kifedha zinazomnufaisha Maduro na mtandao wake wa kifisadi, nazo zitakabiliwa na dhahama kama hiyo. Guaido, alipozungumza na gazeti la wiki la hapa Ujerumani la Der Spiegel aliitaka Ulaya pia kuongeza vikwazo dhidi ya Maduro.
Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa, Michelle Brachellet amesema vikwazo hivyo vinazidi kudhoofisha uchumi ulioharibika wa Venezuela lakini pia kuchochea mzozo wa kisiasa uliosababisha watu milioni 2.7 kukimbia tangu mwaka 2015. Hata hivyo, Guaido amepingana na kauli hiyo ya Brachellet akisema vimewekwa chini ya mwzi mmoja, hivyo haina mahusiano na kudorora kwa uchumi wa Venezuela.
Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE
Mhariri: Bruce Amani