1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Venezuela yaimarisha madaraka ya serikali

17 Mei 2016

Serikali ya Venezuela hapo Jumatatu (16.05.2016) imejipa madaraka makubwa kuhusiana na usalama, ugavi wa chakula na nishati chini ya amri ya hali ya hatari itakayodumu kwa takribani siku sitini.

https://p.dw.com/p/1Ip1Y
Picha: Imago/Agencia EFE/M. Gutierrez

Hatua hizo zilizotangazwa kwenye gazeti la serikali zimeelezea kwa kina tangazo lilitolewa na Rais Nicolas Maduro Ijumaa iliyopita wakati utawala wake ukiwa katika hatari ya kusambaratika kiuchumi.

Venezuela inakabiliwa na mfumuko mkubwa sana wa bei ,uhaba mkubwa wa chakula na umeme na malumbano ya kisiasa kati ya Maduro ambaye amepoteza umashuhuri na bunge jipya linaloongozwa na upinzani ambalo linataka kumng'owa madarakani kwa kupitia kura ya maoni.

Agizo hilo la Maduro linawapa mamlaka wanajeshi kudumisha utulivu wa nchi na kusambaza na kuuza chakula.Kamati za kiraia ambazo hivi sasa zina majukumu ya kugawa chakula pia zitakuwa na mamlaka ya kuwasaidia wanajeshi na polisi kudumisha utulivu wa wananchi na kuhakikisha usalama wa nchi na uhuru wake.

Wahujumu kufungwa

Watu binafsi, makampuni au mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yana mafungamano na taasisi za kigeni yatakuwa yanachunguzwa na fedha zao kutaifishwa iwapo itathibitika kuwa zinatumika kisiasa au zinayumbisha nchi.

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela.
Rais Nicolas Maduro wa Venezuela.Picha: Imago/Xinhua

Hatua hizo pia zinaruhusu kudhibiti bidhaa muhimu au huduma za lazima na kufunguwa njia ya kutaifishwa kwa makampuni.

Akizungumza katika mkutano na wafuasi wake hapo Jumamosi mjini Caracas, Maduro alitishia kuzitaifisha kampuni za watu binafsi ambazo zimesitisha uzalishaji pamoja na kuwafunga wamiliki wa kampuni hizo:

Maduro amesema "Sehemu kubwa ya wafanyabishara nchini humu wanazalisha na wako tayari kufanya kazi hakuna anayepata ushindi hapa. Ndio sababu mtu yoyote yule anayetaka kuihujumu nchi, anapaswa kuondoka. Na yoyote yule anayetaka kuwahujumu wananchi tunatakiwa tuwatie pingu na kuwapeleka gerezani."

Agizo kutathminiwa

Maduro ametowa kauli hiyo siku moja baada ya kutangaza hali ya hatari kupambana na mzozo wa kiuchumi wa nchi hiyo.

Wafuasi wa upinzani wakipambana na polisi wa kuzuwiya ghasia Caracas.
Wafuasi wa upinzani wakipambana na polisi wa kuzuwiya ghasia Caracas.Picha: picture-alliance/Anadolu Agency/C. Becerra

Kwa mujibu wa katiba, agizo hilo linapelekwa kwenye bunge la taifa na Mahakama Kuu kufanyiwa tathmini.

Ingawa wabunge wa upinzani wanatazamiwa kulipinga, lakini huenda likaidhinishwa na Mahakama Kuu, ambapo kuna majaji kadhaa wanaomunga mkono Maduro.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef