1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Venezuela yaigeukia Urusi kuomba msaada

Sylvia Mwehozi
1 Machi 2019

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro ameamuru ofisi za kampuni ya taifa ya mafuta zilizoko mjini Lisbon kuhamishiwa mjini Moscow, mnamo Urusi ikiapa kuendelea kumsaidia rais huyo ikiwa ni pamoja na kutuma misaada ya kiutu. 

https://p.dw.com/p/3EKT1
Russland Moskau Sergey Lawrow empfängt Delcy Rodriguez
Picha: Reuters/M. Shemetov

Makamu wa rais wa Venezuela Delcy Rodrigues amesema hii leo kuwa uamuzi huo wa kuzihamisha ofisi za kampuni ya taifa ya mafuta PDVSA ulilenga katika ulinzi wa mali za nchi hiyo. Aliyazungumza hayo kwenye mkutano wa pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov, akisema Ulaya imeshindwa kuhakikisha usalama wa mali za Venezuela. Aidha alitolea mfano uamuzi wa Benki ya Uingereza kukataa kutoa dhahabu zake akisema sasa Caracas inazidisha ushirikiano na Urusi.

Ofisi ya kampuni ya mafuta ya Venezuela itapanua ushirikiano wa kiufundi katika uchimbaji mafuta na makampuni ya mafuta ya Urusi ya Rosneft na Gazprom. Naye waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema Urusi imetuma msafara wa kwanza wa matibabu nchini Venezuela na pia itaisadia nchi hiyo na misaada ya ngano.

Brasilien Treffen Jair Bolsonaro und Juan Guaido in Brasilia
Juan Guaido na rais wa Brazil Jair BolsonaroPicha: Agência Brasil/A. Cruz

"Kama tunazungumzia hali ya kitu nchini Venezuela kwa ujumla, nafikiri usambazaji wa kiwango kikubwa cha ngano kimesaidia kutuliza hali. Kimesaidia serikali ya Venezuela kushughulikia matatizo yaliyopo.", alisema Lavrov. 

Urusi imetuma jumla ya tani 64,100 za ngano nchini Venezuela hadi kufikia hivi sasa katika msimu wa soko la mwaka 2018/19. Lavrov ameongeza kwamba wamepokea maombi zaidi ya misaada kutoka Venezuela akiongeza kwamba nchi hizo mbili zitaendelea kushirikiana katika nyanja ya masuala ya kigeni. Pia inaituhumu Marekani kwa kujaribu kuchochea mapinduzi dhidi ya rais Maduro.

Urusi kama ilivyo China imekuwa mkopeshaji wa dakika ya mwisho wa Caracas, ikiipatia mabilioni ya dola wakati uchumi wake ukizidi kuporomoka. Pia imeipatia misaada ya kijeshi na katika sekta ya mafuta.

Ikiwa inakabiliwa na mgogoro wa kiuchumi Venezuela ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa wakati kiongozi wa upinzani Juan Guaido alipojitangaza kwa rais wa mpito mnamo mwezi Januari na kusisitiza kuwa Maduro si kiongozi halali. Marekani ilimtambua Guaido na kuongoza kampeni ya kuunga mkono uhalali wake.