1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Venezuela: Maelfu washiriki maandamano kinzani

3 Februari 2019

Kiongozi wa upinzani Juan Guaido awaambia wafuasi wake kutarajia mabadiliko ya haraka wakati mikutano hasimu ikivutia watu 100,000 nchini Venuzuela. Jenerali wa pili wa jeshi akanusha na kupinga mamlaka ya rais Maduro.

https://p.dw.com/p/3Cd8Y
Venezuela Protest & Demonstration gegen Nicolas Maduro in Caracas
Picha: Getty Images/AFP/F. Parra

Kiongozi wa upinzani aliejitangaza kuwa rais wa mpito nchini Venezuela, Juan Guaido, ametoa wito wa "maonyesho ya amani ya nguvu" dhidi ya serikali ya rais Nicolas Maduro, katika juhudzi zake za karibuni zaidi kumlazimisha kiongozi huyo wa kisoshalisti kuachia madaraka.

Vuguvugu la upinzani la Guaido liliandaa maandamano 333 ya kuipinga serikali kote nchini Venuezela, huku tukio kubwa zaidi likifanyika katika mji mkuu Caracas na kuhudhuriwa na watu zaidi ya 100,000.

Waandamaaji hao walitoa wito wa kuondolewa kwa Maduro. Rais huyo wa Venezuela alianza muhula mpya wa miaka sita mwezi Januari, baada ya kushinda uchaguzi wa rais uliozingatiwa na baadhi ya mataifa na jumuiya za kimataifa kukosa uhalali wa kisheria.

Karibu wiki mbili baada ya kujitangaza kuwa kaimu mkuu wa serikali, Guaido aliwaambia wafuasi wake kwamba "mabadiliko yako njiani Venezuela." "Maduro hamlindi yeyote, katiba ndiyo inafanya hivyo," alisisitiza.

Venezuela Caracas Juan Guaido
Juan Guaido akizungumzo katika mkutano wa hadhara mjini Caracas Februari 2, 2019.Picha: picture-alliance/dpa/sincepto/R. Hernandez

Guaido aliitisha maandamano mengine Februari 12, kabla ya kuzungumzia masahibu ya wale walioathirika vibaya na mgogoro wa kiuchumi wa taifa hilo. "Kuna Wavenezuela kati ya 250,000 na 300,000 walioko katika hatari ya kufa," aliuambia mkutano mjini Caracas.

"Leo tunatangaza muungano wa kimataifa wa msaada wa kibinadamu na uhuru nchini Venezuela," Gauido alisema na kuongeza kwamba upinzani utaanza haraka kusambaza msaada kutoka Colombia na Brazil. Aliwahimiza wanajeshi kuruhusu ugavi wa mahitaji muhimu kuingia nchini, ambao Maduro amaeuzuwia mpaka sasa.

Maduro apendekeza uchaguzi wa mapema wa bunge la taifa

Kilomita kadhaa kutoka hapo, Chama cha Maduro cha Kisoshalisti kiliadhimisha miaka 20 tangu hayati Hugo Chavez, mlezi wa kisiasa na mtangulizi wa Maduro alipoingia madarakani. 

Maelfu ya wafanyakazi wa serikali na wafuasi wa Maduro, wakiwemo wanachama wa kundi la wanamgambo wanaoiunga mkono serikali, walikusanyika katika mtaa wa Bolivar katikati mwa Caracas.

Mbele ya wafuasi wake, Maduro kwa mara nyingine alipendekeza kuitisha uchaguzi wa mapema wa bunge mwaka huu. Pendekezo hilo linaonekana kama jaribio la kuwapiku wapinzani, wanaodhibiti bunge la taifa.

Maduro alisema itakuwa juu ya bunge la katiba linaloiunga mkono serikali -- ambalo aliliunda mwaka 2017 ili kudhoofisha nguvu ya bunge la taifa -- kuamua kuunga au kutounga mkono pendekezo lake.

Venezuela Caracas Rede Nicolas Maduro
Rais Nicolas Maduro akiwahutubia wafuasi wake wakati wa kuadhimisha miaka 20 tangu Hugo Chavez alipoingia madarakani.Picha: Reuters/M. Quintero

Muda wa mwisho wa Jumapili kutotimizwa

Mapema wiki hii, mataifa makubwa ya Umoja wa Ulaya yalimpa Maduro muda wa mwisho, na kutishia kumtambua Guaido kama rais iwapo serikali itashindwa kuitisha uchaguzi mpya kufikia usiku wa manane siku ya Jumapili.

Wafuasi wa Guaido wameapa kuzidisha shinikizo dhidi ya Maduro kuelekea muda huo wa mwisho. Mwandamanaji Ziomara Espinoza, mwenye umri wa miaka 59, alisema anahisi mabadiliko ya nguvu miongoni mwa kundi linaloipinga serikali.

"Tuko karibu na uhuru," alinukuliwa akisema na shirika la habari la Associated Press.

Jenerali wa jeshi la anga aasi, amkosoa Maduro

Saa chache kabla ya mikutano hasimu kuanza, afisa wa ngazi wa juu wa kamandi ya juu ya jeshi alikataa mamlaka ya Maduro na kumuidhinisha mpinzani wake. Katika ukanda wa vidio uliosambaa kwenye mtandao wa Twitter, mwanaume alievalia sare alijitambulisha kama Jenerali wa jeshi la anga Francisco Yanez, kabla ya kulaani "mamlaka ya kidikteta na kuchukiza ya Maduro."

"Namtambua Juan Guaido kama rais anaeliongoza taifa la Balivariana la Venezuela," alisema. "Wakati wa demokrasia umewadia," Yanez aliongeza. Jenerali huyo alisema "aslimia 90" ya vikosi vya usalama vilikuwa vinampinga Maduro, na kuwataka raia "kuingia mitaani na kumlinda kwa amani rais wetu Guaido."

Venezuela Krise | mutmaßliches Twitter-Video von Francisco Yanez, Luftwaffe
Jenerali wa jeshi la anga la Venuzuela Francisco Yanez ametangaza kumuunga mkono Juan Guaido.Picha: twiter.com

'Acha aondoke'

Jenerali huyo wa jeshi la anga pia alisema "marafiki wa demokrasia" walikuwa wanamuambia kwamba rais Muduro anaekabiliwa na kishindo "ana ndege mbili zilizo tayari muda wote." Katika vidio hiyo, alitangaza: "Acha aondoke!"

Kamandi kuu ya Venezuela inamuorodhesha Yanez kama mkuu wa kitengo cha mipango ya kimkakati cha jeshi la anga kwenye tovuti yao, iliyo na picha inayofanana na ya mwanaume aliemo kwenye vidio hiyo.

Kwenye ukurasa wake wa Twitter, jeshi la anga la Venuezela lilimshambulia Yanez kama "msaliti" anaenyenyekea madai ya wabepari." Yanez ndiyo ofisa wa ngazi ya juu wa pili kumuidhinisha hadharani Guaido, wiki moja baada ya mwambata wa jeshi wa ubalozi wa Venezuela nchini Marekani Jose Luis Silva kujiuzulu nafasi yake na kutoa wito wa kufanyika uchaguzi mpya.

Jeshi ni nguzo muhimu ya uungwaji mkono kwa Maduro ambaye umaarufu wake umeshuka sana na hadi sasa, limeendeleza utiifu kwa serikali yake. Lakini Guaido alidai kwamba amekuwa na mikutano na viongozi wa jeshi na vikosi vya usalama na kuwashawishi kuhamia upande wake kwa ahadi ya kuwapa msamaha.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/DW

Mhariri: Caro Robi