Uvumilivu kwa Korea Kaskazini umekwisha, Tillerson
17 Machi 2017Waziri Tillerson aliongeza kuwa mbinu kadhaa zinabuniwa ili kukabiliana na taifa hilo lililotengwa.
Tillerson alitembelea mpaka ulio na ulinzi mkali zaidi duniani Ijumaa DMZ, jambo linalomfanya kuwa mmoja wa maafisa wakuu wa Marekani waliotembelea na hata kupigwa picha katika eneo hilo.
Mpaka huo wa DMZ umelindwa pande zote mbili, kukiwa kumetegwa vilipuzi, uzio wenye makali ya wembe, mitego na maelfu ya walinzi waliojihami. Zaidi ya vilipuzi milioni moja vinaaminika kuzikwa katika mpaka huo.
Alipokuwa akizungumza mjini Tokyo awali, waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani aliapa kuweka mikakati mikali ili kukabiliana na kitisho cha nyuklia cha Korea Kaskazini. Lakini hakusema zaidi kuhusiana na yatakayojumuishwa kwenye mwelekeo huo mpya utakaotolewa na Marekani.
Miaka 20 ya diplomasia imeshindwa kuishawishi Korea Kaskazini
"Nataka pia kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wetu wa kihistoria, ushirikiano wetu wa kiuchumi unaozidi kuongezeka na kama ulivyosema, muungano wetu madhubuti wa usalama, kama jawabu kwa kitisho kinachoongezeka cha Korea Kaskazini," alisema Tillerson.
Alisema miaka 20 ya diplomasia na juhudi nyenginezo imeshindwa kuishawishi serikali hiyo ya kikyomunisti kusitisha uendelezaji wa mpango wake wa nyuklia, jambo ambalo Tillerson alilitaja kama kitisho kinachoongezeka kila mara.
Waziri wa mambo ya nje wa Korea Kusini Yun Byung-se aliwaambia waandishi wa habari kuwa nchi yake na Marekani zina lengo moja la kuhakikisha kwamba wanamaliza zana za nyuklia za Korea Kaskazini.
Rais Trump wa Marekani anatafakari kutumia mbinu za kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini
Yun pia amesema mpango wa kujilinda dhidi ya mashambulizi ambao Korea Kusini inautumia unalenga tu kujilinda dhidi ya Korea Kaskazini na wala sio nchi nyengine, kwani China inasema mpango huo unahujumu usalama wake.
Rais Donald Trump anaonekana kutafakari kutumia mbinu zote zikiwepo za kijeshi, ili kusitisha mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini kabla taifa hilo, halijakuwa na uwezo wa kuunda silaha yenye uwezo wa kufika Marekani.
Marekani inaiona China kama nchi muhimu kwa sana iwapo inataka ufanisi wa aina yoyote ile katika kuishawishi Korea Kaskazini, ibadilishe mwenendo wake katika masuala ya Nyuklia, kwani China ndio rafiki wa pekee wa karibu wa Korea Kaskazini mwenye uwezo mkubwa.
Korea Kaskazini imeongeza kasi katika juhudi zake za kuunda silaha za nyuklia, jambo linalokiuka maazimio kadhaa ya Umoja wa Mataifa na taifa hilo linaonekana kutobabaishwa na vikwazo vikali inavyowekewa na jamii ya kimataifa.
Mwandishi: Jacob Safari/AP/DPA/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga