Uturuki yazozana na Ujerumani
3 Machi 2017Uturuki imesema Ujerumani inatakiwa kujifunza kujiheshimu kama inataka kuendeeleza mahusiano kati yao.
Maoni yaliyotolewa na waziri wa masual ya kigeni wa Uturuki, mevlut Cavusoglu yameakisi hatua za awali za kuanza kuvurugika kwa mahusiano kati ya nchi hizo, kwa kuzingatia tukio la hivi karibuni la Uturuki kumkamata mwanahabari wa ujerumani, Deniz Yucel, anaandika mwandishi wa gazeti maarufu nchini Ujerumani la Die Welt.
Waziri wa sheria wa Uturuki Bekir Bodzag alitakiwa kuzungumza na wafuasi wa rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kama sehemu ya hatua zake za kuomba uungwaji mkono kutoka kwa raia wa Uturuki wanaoishi Ujerumani wapatao Milioni 3 katika mchakato wa kura ya maoni utakaofanyika mwezi Aprili wa kumuongeza mamlaka kwa rais wa Uturuki.
Waziri wa masuala ya kigeni wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu, alipozungumza na waandishi wa habari mjini Ankara amesema Uturuki isingeweza kufanya lolote katika mji huo wa Gaggenau, ambako mamlaka ya mji iliondoa kibali cha kufanya mkutano kwa kusema hakuna nafasi ya kutosha katika eneo lililotarajiwa kufanyika mkutano huo.
Meya wa mji wa Gaggenau Michael Pfeiffer amesisitiza kwamba uamuzi huo haukuwa ni wa kisiasa na kusema mji huo ulioko Kusini mwa jimbo la Baden Wuertemberg haukupata maagizo yoyote kutoka kwa mamlaka za juu kusitisha mkutano huo.
Hata hivyo, Uturuki imezungumzia kwa ghadhabu hatua hiyo, kwa waziri huyo wa sheria Bodzag kuhoji "hii nia aina gani ya demokrasia". Akiwa bado katika mji wa mpakani wa Ufaransa, Strasbourg, waziri huyo amesema atarejea nyumbani.
Shirika la habari la serikali ya Uturuki limeripoti kwamba waziri wa sheria wa Ujerumani Heiko Maas aliomba kukutana na Bodzag jana jioni, lakini Bodzag alisema hatahudhuria kikao hicho kutokana na hatua hiyo ya kufutwa kwa mkutano huo. Baadaye Uturuki ilimuita Balozi wa Ujerumani nchini humo Martin Erdmann.
Katika hatua nyingine, mamlaka za mji huo wa Gaggenau uliwahamisha watumishi katika jengo la ofisi za jiji hilo kufuatia kitisho cha bomu kwa njia ya simu. Meya wa Gaggenau Michael Pfeiffer alikiambia kituo cha televisheni cha n-tv siku moja baada ya kufuta mkutano ambapo waziri wa sheria wa Uturuki alitarajiwa kuzungumza.
Alipoulizwa na kituo hicho iwapo kitisho hicho kinaweza kuhusishwa kwa namna yoyote na kufutwa kwa mkutano huo, meya Pfeiffer alisema kwa sasa hivi wanaweza kudhania hivyo, ingawa hawana uhakika. Alisema, tunadhani kuna mahusiano ya moja kwa moja.
Polisi wameendelea kufanya upekuzi kwenye jengo hilo. Na meya huyo amesema, hawajui ni kwa kiasi gani wanaweza kukichukulia kitisho hicho kuwa cha kweli.
Mkutano wa Gaggenau ulikuwa ni moja ya mikutano ya mfululizo iliyopangwa na chama cha tawala cha Uturuki, AKP kufanyika nchini Ujerumani. Wiki iliopita, Waziri mkuu wa Uturuki Binali Yildirim alihutubia wapiga kura wa Uturuki katika mkutano wa kampeni katika mji wa Oberhausen katika mkoa wa North-Rhine Westphalia.
Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE/DPAE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman