Uturuki yawataka waasi wa PKK kufuata Demokrasia
1 Machi 2008ANKARA
Waziri mkuu wa Uturuki RecepTayyip Erdogan amewataka waasi wa kikurdi wa PKK kuweka chini silaha na kufuata njia ya Demkorasia.Wito huo umetolewa muda mfupi baada ya hapo jana kutangaza kwamba vikosi vya Uturuki vimesimamisha opresheni yao dhidi ya waasi hao kaskazini mwa Iraq.
Jeshi la Uturuki limesema katika muda wa wiki moja ya opresheni yao limeweza kufanikiwa kufikia lengo lake.Waziri mkuu Erdogan amesema mashambulio ya wanajeshi wake katika eneo hilo la mpaka wa Iraq limewapa funzo kubwa waasi wa PKK walioko upande wa Iraq.Washirika wa Uturuki ikiwemo Marekani ilitoa mwito kwa nchi hiyo kusimamisha mara moja opresheni ya Kijeshi.Kwa mujibu wa Uturuki waasi 240 wa PKK na wanajeshi wake 24 waliuwawa kwenye harakati hizo wakati waasi wanadai kuwaua zaidi ya wanajeshi 130 wa Uturuki na kupoteza wanachama wake 5 katika mapambano hayo.