Uturuki yawashambulia waasi wa PKK Kaskazini mwa Iraq
24 Oktoba 2007Hali hii ya wasiwasi inajitokeza baada ya hapo jana waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kutoa onyo kali dhidi ya hatua ya Iraqi ya kuchelewa kuwashughulikia waasi hao.Kumekuwepo na ripoti leo hii kwamba wanajeshi wa Uturuki wamefanya tena mashambulio dhidi ya waasi wa PKK katika eneo la mpakani mwa Iraq ingawa maafisa wa serikali ya Uturuki wamekanusha ripoti hizo.
Taarifa zinasemamadege ya kivita ya Uturuki yameshambulia kambi za waasi wa Pkk na kuharibu kila kitu kwenye maeneo ya Sirnak;Hakkari,na Siirt na miko mengine iliyoko karibu na Ira na Iran.Pia inaarifiwa opresheni nyingine za kijeshi zinaendelea katika mkoa wa mashariki wa Tunceli kwa mujibu wa shirika la habari la Uturuki la Anatolia.
Kutokana na hali hiyo vikosi vya ulinzi vya Iraq katika eneo hilo la wakurdi vimeingia kwenye sehemu ya mpaka na Uturuki kwenye mji wa Dahuk kilomita 430 kutoka kaskazini magharibi mwa Baghdad.
Kwa mujibu wa mtu aliyejitambulisha kama kapteini Ziad wanajeshi hao wamefika kwenye eneo hilo kujiweka tayari kuzuia mashambulio ya Uturuki yasiingia Iraq.
Uturuki imewasogeza wanajeshi wake hadi kwenye eneo la mpaka na Iraq baada ya waasi wa Pkk kufanya uvamizi dhidi ya vikosi vyake na kuwauwa wanajeshi 12 na wengine wanane wakatoweka mwishoni mwa Juma.
Waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan akitoa jibu juu ya matokeo ya kaskazini mwa Iraq amesema.
*Ustahamilivu wetu umefikia mwisho wake.Uturuki hivi sasa imejizatiti kuupiga vita ugaidi na ina haki ya kujilinda.*
Hapo jana Uturuki pia ilizionya Iraq na washirika wake wan chi za Magharibi kwamba haiwezi kuondoa uwezekano wa kushambulia kaskazini mwa Iraq hadi pale serikali ya nchi hiyo inayoungwa mkono na Marekani itakapochukua hatua madhubuti kupambana na waasi hao wanaotetea kujitenga.
Katika muda wa wiki kadhaa zilizopita Uturuki imekuwa ikiongeza nguvu ya wanajeshi wake katika mpaka wake na Iraq huku waasi wa PKK nao wakiimarisha mashambulio yao dhidi ya wanajeshi hao wa Uturuki.
Lakini kadri siku zinavyokwenda maji yanaonekana kuzidi unga na kutokana na hali hiyo kumekuwepo na mazungumzo katika sehemu mbali mbali kuujadili mzozo wa sasa.
Mawaziri wa Ulinzi wa jumuiya ya kujihami ya nchi za magharibi Nato pia wanakutana leo hii huko Uholanzi kujadili hali ya mambo katika eneo hilo.
Wakati huohuo rais wa Uturuki Abdullah Gul ataongoza kikao cha baraza la usalama la kitaifa kitakachohudhuriwa na na maafisa wa kijeshi wa ngazi ya juu na mawaziri wa ngazi ya juu.
Lengo la kikao hicho ni kutafakari kwa pamoja ni hatua gani itakayofuatia katika mzozo huu.
Huku hayo yakiarifiwa ujumbe wa Iraq pia umejiandaa kuwa na mkutano hapo kesho na maafisa wa Uturuki kuhusu suala hilo haijatangazwa lakini ni kina nani watakaokuwa katika ujumbe wa Iraq.
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Ali Babacan ambaye alifanya mazungumzo mjini Baghdad hapo jana na viongozi wa juu wa Iraq amesema iraq itawatuma maafisa wake wa ngazi za juu kwa ajili ya kufanya majadiliano na maafisa wa serikali ya mjini Ankara kuhusu hatua zitakazochukuliwa dhidi ya waasi wa Kaskazini mwa Iraq wa Pkk.