Uturuki yataka mwanadiplomasia Brett McGurk aondolewe
18 Mei 2017Taarifa kutoka Uturuki zinasema rais wa nchi hiyo Recep Tayyip Erdogan amemwambia rais wa Marekani Donald Trump kwamba Uturuki itaendelea kupambana na kundi la Kikurdi la Peoples Protection Unit (YPG) nchini mwake hata kama kundi hilo ni mshirika wa Marekani katika kupambana na kundi la kigaidi la IS. Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu ametoa mwito kwa Marekani kumuondoa mkuu huyo wa kikosi chake cha kijeshi kwenye muungano unaopambana na kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS kwa sababu anawaunga mkono wapiganaji wa Kikurdi. Uturuki imeliorodhesha kundi la wapiganaji wa Kikurdi la YPG katika orodha ya makundi ya kigaidi na pia inasema kundi hilo ni kitengo cha chama kilichopigwa marufuku nchini Uturuki cha wafanyakazi wa Kikurdi (PKK) ambacho kinapambana ndani ya Uturuki kwa takriban miongo mitatu sasa.
Mwanadiplomasia huyo maalum wa rais wa Marekani Brett McGurk ameshikilia wadhifa huo wa mkuu wa vikosi vya Marekani kwenye muungano ulio na wanachama 68 tangu utawala wa rais wa Marekani aliyemaliza muda wake Barrack Obama. Muungano huo unapambana na kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS tangu mwaka 2014.
Serikali ya Uturuki inadai kwamba wiki hii McGurk aliwatembelea wapiganaji wa Kikurdi wa kundi la YPG katika eneo la Kaskazini mwa Syria. Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu vilevile amemlaumu mwanadiplomasia McGurk kwa kuendeleza sera za rais wa Marekani aliyeondoka Barrack Obama. Cavusoglu amesema utawala wa rais Donald Trump unaelewa vizuri wasiwasi wa Uturuki juu ya usalama wake na hivyo amemwonya McGurk asiutie sumu utawala mpya wa Marekani kwa kuwaunga mkono wapiganaji wa kundi la YPG. Waziri huyo wa mambo ya nje wa Uturuki amesema Marekani imeihakikishia nchi yake kwamba silaha walizopewa wapiganaji hao wa kundi la YPG zitatumika katika kupambana na IS na wala sio dhidi ya Uturuki na kwamba Marekani imeahidi kuiunga mkono Uturuki katika vita vyake dhidi ya kundi la PKK. Kundi la PKK limeorodheshwa na Marekani na Uturuki katika makundi ya kigaidi. Wakati huo huo kundi la YPG limekanusha madai ya Uturuki kuwa ni mshirika wa kundi la PKK na kuongeza kwamba halitaki mgogoro na serikali ya Uturuki.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan wiki hii alimtembelea rais Donald Trump lakini hakufaulu kumshawishi Trump abadili nia yake ya kushirikiana na wapiganaji wa YPG dhidi ya kundi la IS katika mji wa Raqqa ambao ni ngome ya kundi hilo la kigaidi.
Mwandishi: Zainab Aziz/APE/dw.com/p/2d9op
Mhariri:Yusuf Saumu