Uturuki yataka G20 kuleta ujumuisho zaidi
14 Novemba 2014Uturuki moja kati ya nchi zinazoinukia kiuchumi duniani itakuwa rais wa kundi hilo la mataifa baada ya mkutano huo, ikichukua nafasi ya Australia ambayo ni rais wa sasa. Waziri mkuu wa Uturuki Ahmet Davotoglu amesema nchi yake itatoa umuhimu kwa mataifa yenye kipato cha chini wakati itakapochukua urais wa kundi hilo la mataifa.
Waziri mkuu wa Uturuki Ahmet davutoglu leo ametoa wito wa ujumuisho zaidi katika jukwaa la kundi la mataifa ya G20, akisema hali hiyo itayapa mataifa yenye kipato cha chini sauti imara zaidi , wakati itakapochukua urais wa kundi hilo kwa mwaka 2015.
Uturuki kupanua majukumu ya G20
Davutoglu pia ameashiria kuwa Uturuki itapanua majukumu ya kundi la G20 kupindukia ushirikiano wa kiuchumi na maamuzi hadi katika masuala kama mizozo ya wakimbizi mashariki mwa Ulaya, kuzuka kwa ugonjwa wa Ebola katika bara la Afrika na ugaidi katika mashariki ya kati.
"Wakati wa urais wetu tunataka kuhusisha sauti ya kila mtu," Davutoglu amesema katika mkutano na waandishi habari mjini Brisbane ambako anahudhuria mkutano huo wa viongozi wa mataifa ya G20.
Ajenda ya ujumuisho zaidi ya Uturuki inakinzana na ile ya rais wa sasa Australia, ambayo imejaribu kulazimisha mtazamo wenye mwelekeo mmoja tu kuyahusu makundi mbali mbali kwa ahadi ya kuongeza ukuaji wa jumla wa uchumi wa dunia kwa asilimia mbili za ziada katika muda wa miaka mitano hadi ifikapo mwaka 2017.
Davutoglu amesema Uturuki itaendelea kupigania lengo hilo, lakini imesisitiza umuhimu wa kuzungumzia masuala ya kimaeneo katika mkutano huo.
"Iwapo ajenda za kundi la G20 zitaishia tu katika masuala ya kifedha, kundi la G20 halitaweza kufanya kazi, halitaweza kuwa na uhalali wa kimataifa," ameongeza.
Rushwa pia itajadiliwa
Wakati huo huo rushwa itakuwa mada muhimu pia katika mkutano wa G20, ambapo viongozi wanasema inatishia ukuaji wa uchumi wa dunia, na wanaharakati wanadai kuwa inayaumiza mataifa masikini kwa kiasi kikubwa kwa kuhamisha fedha zinazohitajika sana ambazo zinaweza kutumika kuimarisha mifumo ya afya, shule na barabara.
Prosefa wa sayansi ya kisiasa katika chuo kikuu cha mjini Hong Kong Josepha Cheng hata hivyo anasema Australia imejitahidi kurejesha hadhi ya kundi hilo kimataifa.
"Kuna wasi wasi mkubwa kwamba kundi la G20 huenda linapoteza kasi yake. Mkutano ujao mjini Brisbane ni muhimu kwa kuwa Australia imekuwa ikifanya kazi kwa juhudi kurejesha kasi hiyo, lakini wachambuzi wanahoji iwapo juhudi hizo zinaweza kuleta athari zozote kiasi kwamba watu waweze kurejesha imani yao kwa G20 kama jukwaa la majadiliano na taasisi inayochochea ukuaji wa uchumi duniani na baina ya mataifa yanayoendelea na yaliyoendelea."
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema ana mpango wa kuujadili mzozo wa Ukraine na rais wa Urusi Vladimir Putin katika mkutano huo wa G20 mjini Brisbane.
Uturuki inachukua urais wa kundi hilo mwezi Desemba , wakati uhusiano wake na Marekani na Umoja wa Ulaya ukiathirika kutokana na kukataa kwake kuwa na jukumu kubwa katika kupambana na kundi la Dola la Kiislamu nchini Syria na Iraq.
Bado hata hivyo ina nafasi ya kuwa nchi ya kwanza kuliongoza kundi hilo la mataifa kwa mafanikio kwa muktadha wa taifa ambalo linainukia kiuchumi.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / ape
Mhariri: Gakuba Daniel