Uturuki yaendeleza mashambulizi dhidi ya PKK kaskazini mwa Iraq
28 Februari 2008ANKARA
Uturuki inaendelea na opresheni yake ya kijeshi kaskazini mwa Iraq licha ya kutolewa mwito na Marekani kusimamisha mara moja opresheni hiyo. Uturuki jana ilikataa kutoa ratiba yake ya kuwaondoa wanajeshi katika eneo hilo ambako wanapambana na waasi wa kikurdi wa PKK.
Wanajeshi wa Uturuki wamesema wamewauwa waasi 77 katika mapigano hayo ambayo yamepamba moto,idadi hiyo imefikisha waasi waliouwawa kuwa 230 na wanajeshi 27 wa Uturuki.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani RobertGates ambaye amekwenda Uturuki ameweka wazi kwamba Marekani inaunga mkono washirika wake katika jumuiya ya kujihami ya nchi za magharibi NATO kwamba opresheni hiyo ya kijeshi lazima isimamishwe mara moja.Iraq kwa Upande wake inamsimamo sawa na huo,Waziri wa mambo ya nje Hoshyar Zebari ameuambia ujumbe wa Uturuki uliokwenda Iraq kwa lengo la kutuliza mambo kwamba Serikali ya Iraq inawasiwasi mkubwa juu ya opresheni hiyo na inapendelea Uturuki ikomeshe mapambano hayo ambayo huenda ikaeneza machafuko zaidi ndani ya Iraq.