1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki: Tunasubiri ufafanuzi wa Saudia mauaji ya Khashoggi

Sylvia Mwehozi
13 Novemba 2018

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema nchi yake inamsubiri kwa hamu, Mwana mfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman kutoa ufafanuzi wa kina kuhusiana na mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi.

https://p.dw.com/p/388pt
Türkeiräsident Erdogan berichtet über Audioaufnahmen zum Fall Khashoggi
Picha: picture-alliance/AP Photo/Presidential Press Service

Akizungumza na waandishi wa habari wakati akirejea kutoka katika maadhimisho ya kumbukumbu ya vita ya kwanza ya dunia mjini Paris, Recep Tayyip Erdogan, amesema sauti za mauaji zilizorekodiwa ambazo nchi yake imezitoa kwa maafisa wa Saudi Arabia pamoja na mataifa mengine, ni za "kikatili", kiasi kwamba mmoja wa maafisa wa upelelezi wa Saudia aliyezisikiliza amesema huenda muuaji alikuwa akitumia dawa aina ya heroin.

"Sauti hizo zinatisha. Mmoja wa maafisa wa upelelezi wa Saudia alipozisikiliza, alipigwa na mshutuko na akasema inawezekana mtu huyo alikunywa heroin. Ni mtu pekee aliyekunywa heroin anaweza kufanya hivi", Ni maneno ya Erdogan yaliyonukuliwa na gazeti linalounga mkono serikali la Yeni Safak.

Uturuki inasema mwandishi huyo wa habari aliyekuwa akiliandikia gazeti la Washington Post, na aliyekuwa mkosoaji wa mwana Mfalme aliuawa na timu ya watu 15 wa kitengo cha mauaji waliotumwa kutoka Riyadh. Ankara inasisitiza kwamba maagizo ya kumuua yalitoka ngazi ya juu katika serikali ya Saudia lakini si kutoka kwa Mfalme Salman.

Portraitfoto: Mohammed bin Salman
Mwana wa Mfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin SalmanPicha: picture-alliance/AP/A. Nabil

"Tumetoa mikanda. Tumeipatia Saudi Arabia, Marekani, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza, wote tumewapatia. Wamesikiliza maongezi yote yaliyokuwemo. Wanajua. Hakuna haja ya kupotosha suala hili, wanajua kwamba muuaji au wauaji ni miongoni mwa hao watu 15," alisema Erdogan.

Mwana wa Mfalme anayejulikana kwa kifupi kama MBS, amekuwa chini ya ukosoaji kwa kufahamu mauaji hayo ambayo yalihusisha baadhi ya wanachama wa kikosi chake cha ulinzi. Mwana Mfalme aliueleza ujumbe wa Uturuki kwamba atatoa ufafanuzi wa mauaji hayo na kufanya kila "linalowezekana".

Chini ya shinikizo, Saudi Arabia imejikuta ikibadili maelezo kuhusu mauaji ya Khashoggi. Awali ilisema kwamba mwandishi huyo alitoka nje ya ubalozi siku aliyopotea, lakini baadae ikakiri kwamba Khashoggi alifariki ndani ya ubalozi. Saudi Arabia pia hivi karibuni ilikiri kwamba ushahidi wa Uturuki ulionesha mauaji hayo yalikuwa yamepangwa.

Uturuki inasema timu ya watu 15 kutoka kitengo cha mauaji kilimuua na kuukata kata mwili wa Khashoggi katika ubalozi. Ripoti za vyombo vya habari zinapendekeza kwamba mwili wake huenda uliyeyushwa kwa kemikali kwasababu haujapatikana. Maafisa wa Saudia wanaelezea mauaji hayo kama operesheni ya uhalifu iliyoratibiwa na maafisa wake waliovuka mipaka ya mamlaka.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP

Mhariri: Iddi Ssessanga